MECHI ya kundi D ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco itachezwa saa 1.30 jioni Oktoba 9 mwaka huu nchini Morocco.
Pia Algeria na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambazo pia ziko kundi D zitacheza tarehe hiyo hiyo na muda huo huo ili kuepuka kupanga matokeo. Mechi hiyo itachezwa jijini Algers.
Waamuzi wa mechi kati ya Stars na Morocco watakuwa Gassama Bakary, Jawo Dickory, Touray Sulayman na Camara Bakary, wote kutoka Gambia. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Zoumaro Gnofame kutoka Togo.
Wakati huo huo, mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya African Lyon na Yanga iliyochezwa Septemba 15 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 14,929,000.
Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,038 ambapo kiingilio kilikuwa sh, 7,000 kwa mzunguko na sh. 20,000 kwa VIP. Waliokata tiketi za sh. 20,000 walikuwa 51.
Baada ya kuondoa gharama za mchezo ambazo ni sh. 3,123,409.49 na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 2,277,305.08 kila timu ilipata sh. 3,182,888.47.
Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 1,013,409.49), TFF (sh. 1,013,409.49), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 506,704.75), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 527,643.80) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 101,340.95).