Waziri Prof Mbarawa Akagua Ukarabati Vivuko Dar, Kukamilika Agosti…!
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekagua ukarabati na Ujenzi wa Vivuko vya MV. Magogoni na MV. Pangani na kuwataka wajenzi wa vivuko hivyo kuhakikisha vinakamilika kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kuvikagua Vivuko vya Old MV- Magogoni na Ujenzi wa vivuko vipya vya Pangani na New Magogoni, Prof. Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na hatua za ujenzi zilizofikiwa na kusisitiza kuwa upo umuhimu wa kazi hizo kufanywa hapa hapa nchini badala ya kupelekwa nje ya nchi.
“Hakikisheni mnaongeza nguvu na wataalam ili kazi zote za vivuko na ujenzi wa boti za kuongozea Meli (Tag), zifanyike hapa hapa nchini na hivyo kuokoa fedha nyingi zinazotumika kila mwaka kwa Tug zote saba kukarabatiwa nje ya nchi,” amesema Prof. Mbarawa.
Ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutenga na kujenga eneo maalum litakalotumika kufanyia ukarabati wa vivuko, matishali na boti za kuongozea Meli ili kuboresha huduma ya ufundi katika vyombo vya majini.
“lazima kuwe na mkakati wa kuokoa takribani dola Milioni mbili nukta tano zinazotumika kwaajili ya ukarabati wa Tag zetu kila mwaka,” alisisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), Eng. Le- Kujan Manase amemweleza Prof. Mbarawa kuwa kazi zote za ukarabati wa vyuma na umeme zinafanywa na Mkandarasi kampuni ya M/S Songoro Marine Transport Courtyard ya Mwanza na matengenezo ya Injini na mitambo ya kuendeshea Kivuko yanafanywa na mafundi wa TEMESA na kazi zote zinatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi wa nane.
Kukamilika kwa kivuko cha Old Magogoni na Vivuko vipya viwili vya Pangani na New Magogoni kutaiwezesha TEMESA kuwa na vivuko 30 vinavyotoa huduma hapa nchini na hivyo kuboresha huduma hiyo katika maeneo mengi.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka wenye malori yanayoengeshwa pembeni ya barabara ya kuiingilia Bandarini kutafuta mahali pengine pa kuegesha magari hayo ili kuondoa usumbufu kwa wasafirishaji wanaoingia na kutoka bandarini.
Kivuko kipaya cha Pangani kinatarajiwa kukamilika mwezi septemba na kile kipya cha Magogoni mwezi Oktoba mwaka huu.