CUF wampa pole Rais Dk. Shein ajali ya meli

Mwenyekiti wa CUF, Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
UONGOZI wa Chama Cha Wananchi, CUF umetoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kutoa shukurani kwa juhudi za uokozi zilizochukuliwa na serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein kutokana na kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islander hivi karibuni.

Uongozi wa Chama cha CUF ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake Taifa Machano Khamis Ali, ulifika Ikulu mjini Zanzibar na kueleza kuwa ujio wao huo unawakilisha chama hicho kutoa mkono wa pole kwa Dk. Shein na wananchi wote kwa jumla kutokana na msiba huo mkubwa. Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni pamoja na Wenyeviti wa Wilaya, Mkoa pamoja na viongozi wa wengine wa ngazi mbali mbali.

Alieleza kuwa hali hiyo imewapa moyo mkubwa wananchi kikiwemo chama hicho cha CUF kwa kuona namna kiongozi wao alivyoshiriki kikamilifu katika tukio hilo akishirikiana na viongozi wanzake mbali mbali.

Viongozi hao walieleza kuwa nchi imekuwa na janga kubwa na wao kama ni chama wameona kuna umuhimu mkubwa kuungana na vyama vyengine pamoja na taasisi mbali mbali kutoa mkono wao wa pole.

“Kwa kweli tunakupongeza kwa dhati kwa jinsi ulivyoshiriki kikamilifu katika kutoa huduma katika tukio lile hasa pale ulipomkamata majeruhi mkono na kusaidia na madaktari pale Nungwi”,alisema Machano.

Aidha, uongozi huo ulimueleza Dk. Shein kuwa licha ya juhudi za makusudi zilizochukuliwa na serikali, pamoja na viongozi mbali mbali kuna haja ya kufanywa juhudi za makusudi na serikali katika kuepusha majanga kama hayo yasije kutokea tena.

Uongozi huo pia, ulitoa shukurani maalum kwa serikali kutokana na juhudi za maandalizi zilizochukuliwa katika kipindi kifupi kwa kuwekwa matayarisho kya kutoa huduma katika hospitali ya Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hopitali ya MnaziMmoja pamoja na eneo maalum lililowekwa kwa ajili ya marehemu huko Maisara mjini Unguja.

Mbali ya vituo hivyo, pia walipongeza juhudi zilizochukuliwa za matayarisho kwa ajili ya huduma za lazima katika vituo hivyo wakiwemo wahudumu na madaktari pamoja na dawa. Walieleza kuwa hayo yote yamefanyika kutokana na namna serikali ivyojipanga katika kuwasaidia kwa haraka wananchi wake kutokana na janga hilo.

Nae Dk. Shein, alitoa shukurani kwa ujio wa viongozi hao wa kutoa mkono wao wa pole na kueleza kuwa ni uwamuzi mzuri wa busara.

Dk. Shein alisema kuwa tukio hilo ni la kushtusha kutokana na ukubwa wake na namna lilivyotokea na kueleza kuwa kwa niaba ya wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla amepokea salamu hizo za chama hicho cha CUF.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na ujio wa ujumbe huo na kueleza kuwa tukio hilo ni mitihani ya MwenyeziMungu na licha ya kuwa Zanzibar ni visiwa vilivyozungukwa na bahari lakini tukio kama hilo halijawahi kutokea.

Dk. Shein alieleza kuwa juhudi kubwa za kibinaadamu zimechukuliwa katika zoezi zima la uokozi na hatimae wakapatikana watu waliohai na wengine waliopoza roho ambao waliweza kustiriwa kwa kuzikwa. Aidha, Dk. Shein alisema kuwa tukio hilo litabakia katika historia ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Akieleza kuhusu juhudi za uokozi zilizoendelea kuchukuliwa, Dk. Shein alisema kuwa bado kuna mtihani mkubwa katika suala zima la uokozi kutokana na eneo la tukio kuwa na kina kirefu cha maji kinachokisiwa kuwa zaidi ya mita 380 ambapo pia, ni eneo ambalo lina mkondo mkubwa katika bahari ya Hindi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa juhudi zimechukuliwa licha ya ugumu wa hali ya hewa na umbali wa kina cha maji katika eneo hilo lililozama meli hiyo.

Kutokana na hatua za kuchukuliwa ili tukio kama hilo lisijekutokea tena, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa serikali inaendelea na juhudi zake katika kujadiliana kuhusiana na hali hiyo na kuwahakikishia uongozi huo kuwa suala hilo limezingatiwa..

Dk. Shein alisema kuwa serikali inalifanyia kazi kubwa jambo hilo ili kuhakikisha hatua madhubuti zinawekwa ili kutotokezea tena tukio kama hilo.

Alieleza kuwa licha ya hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuepukana na tukio kama hilo pia, kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuepuka athari za bahari ambazo zinaweza kutokea zikiwemo vimbunga na nyenginezo ambazo huwa zinatokea baharini na kuja nchi kavu.

Dk. Shein pia, aliendelea kuwashukuru wananchi, wakiwemo wananachi na wavuvi wa Nungwi, vyombo vya ulinzi na usalama na Makampuni ya vyombo vya usafiri wa bahari ikiwemo Kampuni ya meliz za Bakhresa kwa kusaidia katika uokozi.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kujipanga vizuri ni lazima na kueleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuyatekeleza yale maelekezo yote yaliotolewa na Baraza la Usalama la Taifa.

Sambamba na hayo, Dk Shein alisema kuwa kuwepo kwa Kitengo cha Maafa pamoja na Kamati ya Maafa pia, ni miongoni mwa mikakati ya serikali katika kupambana na majanga mbali mbali.