Waziri Ataka ‘Data Centre’ ya TTCL Ianze Kazi, Atoa Mwezi Mmoja…!

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitizama kwa karibu mtambo wa kuratibu usalama katika kituo cha kutunza taarifa mbalimbali (data centre) jijini Dar es Salaam. Kituo hicho cha kwanza kujengwa nchini kitatunza taarifa za Serikali na sekta binafsi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akihakiki usahihi wa moja ya kifaa cha kupimia hali ya hewa katika ofisi za Mamlaka hiyo mkoani Singida. Kushoto ni Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa mkoani Singida Bw. Florian Rweyongeza.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa Katibu Mkuu wa Wizara anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL), kuhakikisha kituo cha kutunzia taarifa (Data Centre) kilichopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam kinaanza kufanya kazi.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo kufuatia kukamilika kwa Data Centre hiyo miezi kadhaa iliyopita na mahitaji ya wadau wa huduma ya kutunza kumbukumbu za taasisi zao katika kituo hicho kuongezeka.

“Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano na Mtendaji mkuu wa TTCL hakikisheni kituo hiki kilichojengwa kwa gharama kubwa kinaanza kutumika na kuwezesha mashirika na taasisi mbalimbali kutunza kumbukumbu zao na kuiletea Serikali mapato”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa alisema huduma ya mtandao katika kituo cha Data Centre imeimarishwa kutokana na kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo itawarahisishia wateja wake kuweka na kuchukua taarifa zao kwa haraka.

Akizungumza mara baada ya kukagua maeneo mbalimbali unapopita Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Prof. Mbarawa amemtaka Mkurugenzi wa TTCL kanda ya Kaskazini Bw. Peter Lusama kuhakikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unapitishwa juu ya nyaya katika maeneo yenye changamoto za mafuriko ili kuepuka uharibifu wa mara kwa mara na usumbufu kwa watumiaji.

Aidha amezitaka taasisi za Serikali na binafsi kukitumia kituo cha kisasa cha kuhifadhi taarifa DATA CENTRE kutunza taarifa zao ili kuzihakikishia usalama na uhakika wa kuzitumia wakati wote, ambapo asilimia 75 imetengwa kwa ajili ya kutunza taarifa kutoka sekta binafsi na 25 itatunza taarifa za Serikali.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kulia), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha Ndege mkoani Singida (wa pili kulia), kuhusu mkakati wa Serikali wa ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege kumi na moja ikiwemo kiwanja hicho cha Singida.

Kituo hicho ambacho ni cha kwanza kujengwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni fursa mpya kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali wenye taarifa nyingi kuzihifadhi na kuzitumia wanapozihitaji kinamilikiwa na Serikali na ujenzi wake umegharimu takribani dola za kimarekani milioni 93.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua uwanja wa ndege wa Singida na mahali utakapojengwa uwanja mpya na kusisitiza umuhimu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini kusimamia kikamilifu ujenzi wa uwanja wa ndege wa sasa ambao upembuzi yakinifu wake umekamilika.
Alisema tayari Serikali imebainisha viwanja 11 vya ndege nchini kote na kuvifanyia upembuzi yakinifu kabla ya kuanza kuvijenga ili viweze kukidhi mahitaji ya soko.

Amevitaja viwanja hivyo kuwa ni Lake Manyara, Musoma, Iringa, Tanga, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Simiyu na Singida ambavyo vitapanuliwa na kujengwa kwa kiwango cha lami.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano