*Kutoa elimu nchi nzima kuwalinda raia
Na Joachim Mushi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha ameipongeza Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), kwa kuzindua kampeni ya kupinga unywaji wa pombe kupindukia wa pombe ambao umekuwa na madhara mengi kwa muhusika na Taifa kwa ujumla.
Nahodha ametoa pongezi hizo leo alipokuwa akizindua rasmi kuanza kwa kampeni hizo nchini, ambapo SBL itaanza kutoa elimu kwa wananchi kote kuhakikisha wanakunywa pombe kistarabu ili kulinda hadhi yao na familia zao.
Waziri huyo amesema kila kitu kinapotumiwa bila ustarabu kinakuwa na madhara, hivyo ameguswa na kitendo cha SBL ikiwa moja ya makampuni yanayotengeneza pombe kufanya uamuzi wa kuanza kuwalinda wateja wake na Watanzania wote kuhakikisha wanatumia vivyaji vywa kampuni hiyo kiustarabu.
“Mimi nawashukuru sana Kampuni ya Serengeti kwa kuanzisha kampeni hizi…hii inaonesha ni namna gani mnavyoyajali maisha ya wateja wenu na raia wote. Unywaji wa pombe bila ustarabu unamadhara makubwa kwa mnywaji na wengine, japokuwa mnywaji ndiye mwenye manufaa zaidi.
Aidha akifafanua zaidi amesema utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Shule ya Uandisi na Teknolojia mwaka 2007 umebaini kwa mwaka 2006 zilitokea ajali 17,677 kati ya hizo vifo vilikuwa 2,838 na majeruhi 15,855. Anasema ajali hizo zimelipa hasara taifa kwa takriban sh. bilioni 508.
“Ukiangalia asilimia 76.4 ya ajali hizi zimesababishwa na makosa ya kibinadamu ikichangia na pombe…sasa unywaji wa kistarabu utatusaidia,” alisema Waziri.
Akizungumza awali Mkurugenzi wa Mawasiliano wa TBL, Bi. Teddy Mapunda amesema kampuni yao imetenga kiasi cha sh. milioni 352 ambazo zitatumika kutoa elimu ya unywaji wa pombe kistarabu kupitia matangazo, warsha, makongamano na hasa kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao (Blogs, Website n.k).
“Kimsingi unywaji wa pombe kupita kiasi (bila ustarabu) ni mbaya sana kwani Taifa linapata hasara watu wanashindwa kutimiza wajibu wao wanaathiri vipato vyao na taifa…lakini mtu akinywa kistarabu ataweza kuwajibika. Huu utakuwa ni mkakati wa aina yake tutaweka mabango nchi nzima na kwenye magari yote ya abiria ili eli hii imfikie kila mmoja,” alisema Bi. Teddy.
Sambamba na hayo SBL imelikabidhi Jeshi la Polisi nchini vifaa maalumu ambavyo vitatumika kupima kiwango cha ulevi kwa madereva, ambavyo vinagharimu kiasi cha sh. milioni 25.