Boss TANAPA na Mchungaji TAG ‘Mbaroni’ Kukutwa na Jino la Tembo

Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi akizungumza.

Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi akizungumza.

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) linamshikilia Mhifadhi Mwandamizi wa shirika hilo baada ya kuhusishwa na tukio la mchungaji kukamatwa na jino la tembo alilokuwa akilinadi kutafuta mteja.

Kwa mujibu wa taarifa ya TANAPA kwa vyombo vya habari, bosi anayeshikiliwa ni Genes Shayo baada ya mchungaji, wa Kanisa la TAG, Emmanuel Nassari (46) Wilaya ya Arumeru kukamatwa na jino hilo na kikosi maalumu cha kupambana na ujangili na kisha kumtaja bosi huyo kuwa anahusika na nyara hiyo.

“Kikosi kazi hiki mara baada ya kupata taarifa hizi kiliendelea na taratibu zake za kiuchunguzi na baada ya ufuatiliaji walifanikiwa kumkamata Emmanuel Nassari tarehe 15/05/2016 akiwa na jino moja la tembo ambapo katika mahojiano yaliyofanyika alimhusisha Mhifadhi Mwandamizi wa TANAPA Genes Shayo kuwa anazo taarifa za yeye kuwa na jino hilo na hivyo kukamatwa tarehe 16/05/2016 kwa ajili ya mahojiano zaidi,” ilisema taarifa hiyo ya TANAPA.

TANAPA inawaomba wananchi wema kuendelea kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na ujangili kwa lengo la kuchukuliwa hatua ili kudhibiti vitendo hivyo haramu kwa taifa.