Serikali yasitisha kazi ya kutafuta maiti majini

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa tamko la kusitishwa rasmi shughuli ya utafutaji wa miili ya watu walionasa kwenye meli ya Mv. Spice Islanders iliyozama eneo la Nungwi Kaskazini mwa Kisiwa cha Unguja, Zanzibar kutokana na ugumu wa utekelezaji wa kazi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, imesema kusitishwa kwa shughuli hiyo kunatokana na wazamiaji kutoka Afrika Kusini kushindwa kuifikia meli hiyo kutokana na kina kirefu eneo la ajali pamoja na hali mbaya ya hewa.

Akitangaza uwamuzi huo wa Serikali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Iddi, amesema ingawa Serikali ilikuwa na nia ya kutaka kutolewa kwa kila mwili ulionasa kwenye meli hiyo, lakini imebainika kazi hiyo ni ngumu kutekelezeka.

Aidha amewaomba Watanzania kukubali kuwa ndugu zao waliopoteza maisha na miili yao kushindikana kupatikana ni mapenzi na maamuzi ya Mwenyezi Mungu aliyeamua kuwa bahari iwe sehemu ya makaburi ya ndugu zetu hao.

Balozi Iddi amesema kila mmoja hana budi kumshukuru Mungu na kukubaliana na hali hiyo kwani hata Serikali ingekuwa na nia ya kuendelea na kazi hiyo ingechukua muda mrefu na mwisho wa siku huenda pia isifanikiwe.

Lakini pia Balozi Iddi, amesema tangu kuzama kwa meli hiyo hadi leo ni muda mrefu kiasi ambacho hata kama miili ingefanikiwa kutolewa isingekuwa rahisi kutambulika kutokana na kuharibika vibaya.

Katika hatua nyingine Balozi Iddi amesema kuwa taarifa zote zinazohusu tukio hilo zitatolewa na ofisi yake ama kupitia kwa Waziri wa nchi katika ofisi yake, Mohammed Aboud ili kuepuka utoaji wa taarifa za kuwachanganya wananchi.