MAJERUHI wa ajali ya basi la Grazia lenye namba za usajali T 591 ADK linalofanya safari zake kati ya Njombe na Dar es Salaam wamenusurika kufa mbele ya spika wa bunge la jumhuri ya muungano wa Tanzania na baadhi ya viongozi wa CCM na wakuu wa wilaya wakati akisubiri bila mafanikio gari ya wagonjwa kutoka Hospitali ya mkoa wa Iringa umbali wa kilometa kama 8 hivi hadi eneo la ajali .
Kutofika kwa Ambulence hiyo ya wagonjwa katika eneo hilo la ajali kwa ajili ya kusaidia kukimbiza majeruhi Hospitali kulimlazim spika huyo wa bunge Mhe. Anna Makinda kusitisha ziara yake kwa muda na kulazimika kusaidia kuokoa maisha ya majeruhi hao kwa kusaidiana na wabunge ,wakuu wa wilaya pamoja na mkuu wa kikosi cha usalama mkoa wa Iringa (RTO) Kedmund Munubi kwa kuamua kutumia gari ya mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa (CCM) Lediana Mng’ong’o kama gari ya wagonjwa .
Ajali hiyo ilitokea leo majira ya saa 3.10 asubihi katika eneo la Mseke mpakani mwa wilaya ya Iringa vijijini na Manispaa ya Iringa wakati basi hilo likitokea wilayani Njombe kwenda jijini Dar es Salaam kabla ya kupinduka wakati dereva wa basi hilo akijaribu kulikwepa Lori bovu mbele na hivyo usukani kumshinda na basi hilo kuhama njia na kupinduka.
Deo Mwinuka ambaye ni moja kati ya abiria walionusurika kifo katika ajali hiyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kuwa dereva wa basi hilo Dominic Castori alishindwa kulinudu basi hilo kutokana na mwendo mkali aliokuwa akiendanao .
“Kwanza ukitazama eneo hili ni mteremko ila bado dereva wetu alitaka kulazimisha kulipita lori bovu lililokuwa limeegeshwa katikati ya barabara na baada ya kubaini kuwa lori hilo ni bovu ndipo alipolitoa basi hilo nje ya barabara na kupinduka”
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Mng’ong’o aliueleza mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kuwa wakati ajali hiyo inatokea yeye alikuwa umbali wa kama mita 100 hivi akishuhudia jinsi ambavyo basi hilo linavyoyumba na mbele kulikuwa na kijana mwendesha baiskeli ambaye aliamua kuruka katika baiskeli yake na kukimbia kuokoa maisha yake.
Hata hivyo alisema kuwa baada ya basi hilo kuanguka alifika eneo hilo la ajali na kuanza kusaidia kuwavuta majeruhi wa ajali hiyo huku akikemea vibaka wasiibe mizigo ya majeruhi hao.
Mbunge huyo alisema kuwa akiwa katika jitihada`za kuendelea kuokoa majeruhi mkuu wa wilaya ya Njombe Sarah Dumba alifika na kuungana naye kusaidia majeruhi pamoja na kupiga simu kwa mganga mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Iringa Dkt Ezekiel Mpuya na DKT kushuma ili kuomba msaada wa haraka wa gari ya wagonjwa ila hadi majira ya saa 4..30 msafara wa spika Makinda unafika eneo hilo la ajali hakuna msaada wowote wa madaktari wa Hospitali ya mkoa ambao walikuwa wamefika eneo hilo.
Hata hivyo mwandishi wa habari hizi alishuhudia mkuu wa wilaya ya Mufindi Evarista Kalalu na watu wa usalama wa Taifa wakiendelea kupiga simu katika Hospitali ya mkoa wa Iringa ili kuomba msaada wa haraka wa gari ya wagonjwa bila mafanikio jambo lililomlazimu spika Makinda kuagiza gari ya mbunge Mngongo ishushe bendera na itumike kubeba majeruhi wa ajali hiyo pamoja na gari ya polisi.
Akitoa pole kwa majeruhi hao Makinda aliwataka majeruhi kuendelea kuwa wavumilivu zaidi na kujipa moyo na kusahau tukio hilo huku akiwahakikishia kuwa asingeweza kuendelea na ziara yake katika kijiji ha Tanangozi kabla ya majeruhi hao haajasaidiwa eneo hilo.
Mganga mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Iringa Dkt Mpuya hakuweza kupatikana kuzungumzia sababu ya gari hilo la wagonjwa kushindwa kutokea eneo la ajali kusaidia majeruhi japo simu yake ilionyesha kuita bila kupokelewa .
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwa jumla ya majeruhi watano ndio waliojeruhiwa vibaya katika ajali hiyo na kuwa watatu wamelazwa katika Hospitali ya mkoa wa Iringa huku wawili wametibiwa na kuruhusiwa.
-Habari na picha kwa hisani ya Godwin Blog