Azam Waachana na Stewart Hall

1

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo imeachana rasmi na aliyekuwa Kocha Mkuu wake, Stewart Hall, baada ya kufanyika makubaliano ya pande zote mbili.

Uongozi wa Azam FC umechukua hatua hiyo kufuatia hivi karibuni Hall kutangaza uamuzi wa kuachia ngazi akiweka wazi kuwa amechoka kufundisha soka Tanzania na sasa anataka kwenda kutafuta changamoto nyingine mpya ya kufundisha soka nje ya nchi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema mara baada ya kukaa meza moja na Hall wamekubaliana kwa pamoja juu ya ombi lake hilo huku akieleza kuwa kwa sasa kikosi hicho kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi.

Alisema Kitambi atakinoa kikosi hicho katika mechi mbili zilizobakia msimu huu, ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT itakayofanyika Jumapili hii (Mei 22) pamoja na ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) watakayokipiga na Yanga Juni 11 mwaka huu.

“Leo tumeachana na Hall kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya kutuomba kuachia ngazi kwa lengo la kutafuta changamoto nyingine nje ya nchi, wakati tukijipanga kuunda benchi jipya la ufundi kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi hadi kumalizika kwa msimu huu,” alisema.

Kawemba pia alichukua fursa hiyo kumpongeza Hall kwa mafanikio aliyoipa timu hiyo kwa muda mchache aliofanya kazi ndani ya Azam FC huku akimtakia kila la kheri katika timu nyingine atakayokwenda kuifundisha.

“Tunamshukuru Hall kwa mafanikio aliyotupa msimu huu, kwanza kutupa ubingwa wa Kombe la Kagame, kuingia fainali ya Kombe la FA na sasa tukiwa nafasi ya pili kwenye ligi, hii ni rekodi nzuri na tunamshukuru sana kwa hilo na tunapenda kumtakia kila la kheri katika timu nyingine atakayokwenda kufundisha,” alisema.

Rekodi ya Hall Azam FC
Kocha huyo raia ya Uingereza aliyeifundisha Azam FC kwa nyakati tatu tofauti, tokea aanze kibarua hicho Juni mwaka jana anaondoka akiwa ameinoa timu hiyo katika jumla ya mechi 62 msimu huu, akishinda mara 41, sare 16 na kufungwa mechi tano.

Katika idadi hiyo ya mechi, Hall ameiongoza Azam FC kufunga jumla ya mabao 111 na kufungwa 41, huku akimaliza mechi bila kufungwa bao lolote (cleensheet) ndani ya michezo 31 pekee.

Chanzo:www.azamfc.co.tz