Kamishna wa polisi wa mji wa Manchester ameitisha uchunguzi kuhusiana na bomu bandia lililoachwa katika uwanja wa Old Trafford baada ya zoezi la mafunzo na kusababisha kufutwa mchuano wa ligi kuu ya kandanda ya England
Kifaa hicho kilisababisha watu kuondolewa katika uwanja huo wa Manchester United muda mfupi kabla ya kuanza mchuano wao wa mwisho wa msimu dhidi ya Bournemouth.
Kamishna wa Polisi wa mji wa Manchester Tom Lloyd amesema kisa hicho kilisababishan usumbufu mkubwa kwa mashabiki waliotoka sehemu za mbali kuja kutazama mpambano huo.
Mchuano huo umepangwa kuchezwa upya hapo kesho Jumanne, lakini matumaini ya Manchester United kufuzu katika kandanda la Champions League msimu ujao ni sifuri baada ya Manchester City kumaliza katika nafasi ya nne jana kwa kutoka sare ya bao moja kwa moja na Swansea City. United pia watapambana na Crystal Palace katika fainali ya Kombe la FA siku ya Jumamosi.
Chanzo:dwswahili.com