MKURUGENZI Msaidizi wa Sheria na Uanachama wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF), Eliud Peter Mvela, ametoa siku mbili kwa uongozi wa chama cha soka Mkoani Arusha (ARFA) kutoa tamko juu ya malalamiko yanayohusu ligi daraja la tatu ngazi ya Mkoa huu iliyomalizika Mwishoni mwa mwezi wa tatau mwaka huu
Kauli hiyo inakuja juu ya Mkurugenzi huyo kukutana na uongozi wa ARFA Pamoja na baadhi ya viongozi wa timu zilizoshiriki ligi ya mkoa na kukubaliana na kuipa ARFA Itoe maamuzi yenyewe ndani ya siku walizopewa
“Endapo ARFA watashindwa kutoa maamuzi au wakatoa maamuzi ambayo hayalidhishi kutokana na ukubwa wa tatizo basi TFF tutalisimamia wenyewe na kwa kuonesha mfano tutaanza kwa aibu hii iliyotokea Arusha itakuwa mfano kwa wengine” alisema Mvela
Katika kikao hicho kilichochukua zaidi ya masaa mawili, ambacho waandishi wa habari hawakuruhusiwa kutokana na sababu zisizojulikana, viongozi wa vilabu walionekana kujawa na faraja kuja kwa kiongozi huyo huku wachache wakiingiwa na wasiwasi
“Tulijua Mvela amekuja kumaliza kabisa swala hili na sio kusikiliza nini kimetokea kama alivyofanya na kuhaidi kulitatua mapema, hii najua ni danganya toto mwisho wa siku hakuna kitakachofanyika maana tumeshuhudia viongozi wengi wakija lakini hakuna hatma” alisema mmoja wa viongozi waliohudhulia kikao hicho ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mvela aliongeza kuwa timu nyingi ziliingia kwenye mashindano kichwa kichwa bila kujua kanuni za mashindano na mwisho wa siku hawajui wafanye nini na hajui anatakiwa afanye nini na kwa nani
Aliongeza kuwa ili kuingia kwenye mashindano yoyote lazima timu ziwe na kanuni na tatizo hilo sio mikoani kuna timu ambazo zipo ligi kuu lakini hawajui kanuni za ligi na ndio maana kila kukicha adhabu zinajitokeza, kwani viongozi na wachezaji wengi hawasomi kanuni
”Viongozi wa vilabu walikuwa wanalalamika bila kupeleka barua kwa viongozi hivyo kulikuwa hakuna hoja ya wao kuwasaidia kwa kuwa malalamiko hayakuwa kiofisi, lakini wameniambia wamepata barua wiki iliyopita na ARFA Wamenihaidi kutoa tamko” alisema Mvela