Askari wa Bunge Achomwa Kisu na ‘Kichaa’

Askari wa Bunge Achomwa Kisu na 'Kichaa'

Askari wa Bunge Achomwa Kisu na ‘Kichaa’

MTU anayesadikiwa kuwa na upungufu wa akili amemchoma kisu mmoja wa askari wa Bunge la Tanzania. Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari mtu huyo aliyewasogelea ghafla askari polisi ambao walikuwa mchanganyiko na askari wa bunge ghafla alimchoma kisu cha kifua mmoja wa askari wa Bunge kabla ya kudhibitiwa na askari Polisi.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa kumi jioni wakati vikao vya bunge vikiendelea katika moja ya geti la eneo la kuingilia bungeni mjini Dodoma. Chanzo cha habari kilibainisha mtu huyo jinsia ya kike aliwasogelea askari kana kwamba alikuwa akihoji jambo kabla ya kutoa kisu ghafla alichokuwa amekificha na kumchoma askari huyo ambaye alianguka chini kabla ya kuanza kupewa msaada na wenzake.

Tayari Jeshi la Polisi linamshikilia mwanamama huyo kwa uchunguzi zaidi ikiwemo kumfikisha katika vyombo husika kupimwa akili. Askari aliyechomwa kisu alipewa msaada wa huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi. “…Bahati nzuri kisu alichochomwa hakikuingia sana maana alifikishwa hospitalini na baada ya matibabu ya awali alianza kuzungumza na sasa bado anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri,” kilisema chanzo cha habari.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo. dev.kisakuzi.com inaendelea kumtafuta aweze kuzungumzia zaidi tukio hilo.