Serikali kupitia Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo imesitisha kuchezwa kwa wimbo na video ya Chura ya msanii Snura Mushi kwenye vyombo vyote vya habari nchini mpaka itakapofanyiwa marekebisho.
Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini na msemaji wa Wizara ya Habari Zawadi Msalla alisema video ya wimbo huo inadhalilisha utu wa mwanamke na inaifanya jamii ianze kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya sanaa kwa ujumla.
“Tumeufungia wimbo na video yake kuchezwa redioni, kwenye runinga, baa au sehemu yoyote ya wazi na yenye mkusanyiko wa watu wengi.
” Tunamtaka Snura aitoe video hiyo YouTube mara moja ili isiendelee kutazamwa na watu wengi kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,”alisema Msalla.
Aidha Serikali inawakumbusha wananchi wote kutojiingiza katika makosa ya mtandao kwa kusambaza wimbo huo kwa njia yoyote ile ya mtandao.
Pia Serikali inavitaka vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya sanaa kabla ya kuwa mawakala wa uharibifu kwa jamii kupitia kucheza kazi chafu za wasanii.
Wakati huo huo Serikali imemfungia msanii Snura kujihusisha na masuala ya muziki mpaka atakapojisajili katika Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).