AJALI ya ndege nchini Angola imesababisha vifo vya watu 26, wakiwemo majenerali wa kijeshi watatu, Ofisa wa Serikali ameiambia BBC. Luis Caetano, Msemaji wa Mamlaka ya Jimbo la Huambo, amesema ndege hiyo ya kijeshi ilianguka baada ya kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa Huambo. Amesema watu sita wameokoka kwenye ajali hiyo, akiwemo rubani na msaidizi wake.
Waandishi wa habari wamesema ni ndege mpya ya muundo wa Embraer iliyonunuliwa na jeshi kusafirisha maofisa waandamizi. Taarifa za awali zilisema kuwa kulikuwa na abiria 36 ndani ya ndege, lakini Caetano ameiambia BBC walikuwepo 32.
Alisema ndege hiyo ilipasuka ilipopata ajali hiyo na miili ya watu 26- 20 ya wanaume na sita ya wanawake iliopolewa. Watu waliokuwa wamekaa sehemu ya mbele ya ndege hiyo walinusurika, lakini waliokaa nyuma walifariki dunia kutokana na upande huo kushika moto.
Bw Caetano alisema, mmoja wa walionusurika aliungua sana na alikuwa akipata matibabu hospitalini. Alisema, rubani aliyezungumza na televisheni ya Angola, alionekana kuchanganyikiwa lakini alisistiza kuwa alifuata masharti yote aliyopewa.
Mmoja wa walionusurika alinukuliwa na gazeti la Sol akiwa hospitali akisema ajali hiyo ilitokea haraka kiasi cha kushindwa kujua tatizo ilikuwa ni nini, lakini rubani alionekana kufahamu kwamba kulikuwa na tatizo la kiufundi.
-BBC