KCB yatoa msaada wa vifaa vya hospitali

Meneja wa KCB Tanzania Tawi la Mwanza Walter Lema, akimkabidhi Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Joseph Batholomeo sehemu ya vifaa vilivyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya wodi ya wazazi vyenye thamani ya Milioni 4.9/-. Anayeshuhudia nyuma yao ni Meneja Mikopo wa KCB Tanzania Baguma Kifumbe.

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

BENKI ya KCB Tanzania imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vikiwemo vya tiba kwa hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, iliyopo Butimba ya jijini Mwanza ili kusaidia akinamama wanaojifungua.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 4,9/- vilikabidhiwa kwa uongozi wa hospitali hiyo na Meneja wa tawi la Mwanza, Walter Lema na kupokekelewa na Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali hiyo Joseph Batholomeo.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Lema alisema KCB Tanzania kwa kuthamini afya za binadamu na wananchi wa Jiji la Mwanza imetoa msaada huo ili kuwezesha kutolewa kwa huduma bora za afya kwa wazazi na wananchi wengine.

Alisema KCB inatambua umuhimu wa huduma za afya na kwamba wananchi kama wadau wa benki hiyo wakipata huduma bora zinazokidhi wataweza kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli za uzalishaji na kujiingizia kipato.

“KCB Tanzania kama chombo cha fedha wadau wetu wakubwa ni wananchi, ambao bila kuwa na afya njema hawawezi kufanya shughuli za uzalishaji, kadhalika hata sisi tutakuwa tumeathirika, msaada huu kwa hospitali hii umelenga kurudisha faida kwa wadau wetu waweze kupata tiba bora na uhakika” alisema Lema

Kutokana na hilo alibainisha kwamba benki hiyo itaendelea kutoa misaada yenye tija kwa hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha miundo mbinu yake na kuwezesha madaktari kutoa huduma bora.

Aidha aliwaasa wananchi na watumishi wa hospitali hiyo kujiunga na benki hiyo kwa vile huduma zake zimesambaa katika nchi za Afrika Mashariki ambapo kwa hapa nchini inayo matawi 11.

Kwa upande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali hiyo Joseph Batholomeo mara baada ya kupokea vifaa hivyo ambavyo ni kwa ajili ya wodi ya wazazi alisema kwa kutambua mahitaji ya jamii wanayoihudumia, vifaa hivyo vitaongeza ufanisi wa huduma wanazozitoa.

Alisema utakuwa chachu ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi na ni vema watumishi wa hospitali hiyo wakiwemo madaktari na wauguzi wakajiunga na benki ya KCB Tanzania kwa kufungua akaunti ili kuunga mkono juhudi zao za kusaidia jamii kutokana na faida zinazotokana na wateja wa benki hiyo.

Vifaa vilivyotolewa ni Vitanda viwili vya kujifungulia, mashine tano za kupima joto, mashine mbili za kupimia uzito, vitambaa vya kukinga wagonjwa (usiri) wakati wa kutoa tiba watatu, magodoro matatu, makoti mawili ya watoto wanaozaliwa , makasha tatu ya kuhifadhia uchafu kwa vifaa tiba vilivyokwishatumika, vifaa vya kuzalishia na Aprona tano. Vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 4,935,000.