POLISI wa kupambana na ufisadi nchini Nigeria, wamenasa saa yenye thamani ya takriban dola za Kimarekani milioni moja nyumbani kwa aliyekuwa Waziri wa zamani wa Wizara ya Mafuta Nigeria ambaye pia anachunguzwa kufuatia tuhuma za ufisadi.
Saa hiyo ya kipekee ni moja kati ya vitu mbalimbali bvya mapambo ya dhahabu, almasi na fedha vilivyonaswa katika operesheni hiyo ya kushtukiza katika nyumba ya aliyekuwa waziri wa mafuta wa Nigeria katika utawala uliopita, Bi. Diezani Madueke.
Shirika la kupambana na ufisadi la Nigeria (Economic and Financial Crimes Commission) limethibitisha kuwa Bi. Madueke anachunguzwa kufuatia madai ya ufisadi. Taarifa zinasema mabilioni ye fedha yalitoweka katika wizara yake pindi akiwa madarakani.
Taarifa zinasema fedha hizo zilikuwa sehemu ya mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta katika soko la kimataifa. Mwaka uliopita, Bi. Madueke alikamatwa na kuhojiwa na maafisa wa upelelezi wa Uingereza lakini akaachiwa kwa dhamana.
Rais mpya wa Nigeria, Muhammadu Buhari alichaguliwa kwa nia ya kumaliza kabisa ufisadi uliokuwa umekithiri nchini humo. Rais Muhammadu ameahidi kutokomeza kabisa ufisadi.
Baada ya maofisa wa kupambana na ufisadi nchini Nigeria kutangaza kuwa wamenasa mapambo anuai yenye thamani ya dola milioni 2 nyumbani kwa aliyekuwa waziri wa mafuta wa nchi hiyo, Bi. Diezani Alison Madueke watu wengi wameelezea mshangao wao kutokana na thamani hiyo ya juu ya saa hiyo. Wengi kupitia kwa mitandao ya kijamii wanahoji itakuwaje saa inagharimu fedha za aina hiyo ?
Kwani saa hiyo imeundwa na nini?
Utafiti wetu umebaini vitu vitatu.
1.) Saa yenye thamani ya juu sharti iwe na sehemu zilizoundwa na mawe yenye thamani ya juu kama vile Almasi, Platinum, dhahabu, na mawe kutoka anga ya mbali.
2.) Saa hiyo lazima iwe imechukua muda mrefu sana kuitengeneza na iwe na uwezo wa kufanya kazi bila hitilafu ya mara kwa mara.
3.) Saa hiyo pia lazima iwe na uwezo wa kipekee wa kutekeleza majukumu yake mbali na kueleza wakati
Hivyo ndivyo vipengee tatu muhimu ambavyo vinajirejelea katika orodha ya saa tano ghali zaidi duniani mwaka huu wa 2016 kulingana na jarida la saa ghali zaidi la ALUX.
-BBC