Na Mwandishi Wetu
SALAMU za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islanders na kuua watu 202 zimezidi kumiminika nchini kutoka Jumuia ya Kimataifa.
Salamu hizo za rambirambi pia zimetumwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein.
Hadi leo, Septemba 14, 2011, Rais Kikwete alikuwa ametumiwa salamu za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali 22.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu iliyotolewa leo inazitaja sehemu hizo ni pamoja na kutoka kwa Mfalme wa Sweden, Carl Gustaf R, Gavana Mkuu wa Canada, David Johnston, Waziri Mkuu wa Mauritius Dk. Navinchandra Ramgoolam na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Salamu nyingine zimetumwa kutoka nchi za Benin, Philippines, Ukraine, Poland, Belarus, Misri, na Khazkistan. Aidha, nyingine zimetumwa kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mama Asha Rose Migiro, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mohammed Babu, Balozi wa Tanzania katika Ufaransa Mama Begum Karim Taj, na Balozi wa Tanzania katika nchi za Misri, Ali Shauri Haji ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika Israel, Jordan, Libya, Lebanon, Syria na Palestine.
Taarifa hiyo pia imeeleza, Rais Kikwete amepokea salamu za rambirambi kutoka kwa Kaimu Balozi wa Tanzania katika Oman, Abdallah Abasi Kilima, Balozi wa Tanzania katika India Mhandisi John H. Kijazi, Balozi wa Tanzania katika Canada, Alexander C. Masinda na Balozi wa Tanzania katika Brazil, Francis Malambugi.
Salamu pia zimepolekewa kutoka kwa Katibu Mtendaji wa International Conference on the Great Lakes Region Balozi Liberata Mulamula na kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mazao (Common Fund for Commodities), Ali Mchumo.
Meli ya Spice Islander ilizama kwenye pwani ya Zanzibar katika eneo la Nungwi usiku wa kuamkia Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, 2011 na mpaka sasa watu 202 wamethibitishwa kuwa walipoteza maisha katika ajali hiyo na wengine 619 waliokolewa katika ajali hiyo.
Hadi sasa meli hiyo iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Pemba kupitia Zanzibar haijaweza kuopolewa kutoka baharini hata kama wazamiaji wa ndani na kutoka Afrika Kusini wanaendelea na kazi ya kuitafuta meli hiyo.