Serikali Yaunda Kamati Kuanzisha Tume ya TEHAMA

Wajumbe wa Kamati ya mpito ya kusimamia uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika picha ya pamoja.

Wajumbe wa Kamati ya mpito ya kusimamia uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika picha ya pamoja.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, ameunda Kamati ya mpito ya kusimamia uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo ameipa miezi sita kufanya kazi kuanzia mwezi Aprili, 2016 ya kuhakikisha kuwa Tume ya TEHAMA inaanza kazi rasmi.

Katika kuhakikisha kuwa Tume ya TEHAMA inaanza kazi mara moja, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano, Prof. Faustin Kamuzora, amewakabidhi wajumbe wa Kamati hiyo Amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na.532 iliyotolewa kupitia gazeti la Serikali Na. 47 la tarehe 20 Novemba, mwaka 2015 iliyoanzisha Tume na Hadidu za Rejea zinazoainisha majukumu yao. Majukumu hayo ni pamoja na kusimamia uanzishwaji wa Tume, kuandaa sheria ya kuanzisha Tume, na kutengeneza Mpango Mkakati wa Tume. Prof. Kamuzora amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuepuka kuweka mitazamo au maslahi binafsi ya wao wenyewe au ya taasisi zao katika kipindi cha kuanzisha Tume, bali waishauri Serikali namna nzuri ya kuhakikisha kuwa Tume hiyo inaanza kazi ya kusimamia na kuratibu masuala ya TEHAMA nchini. Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao na Katibu wa Kamati ya Kuanzisha Tume ya TEHAMA nchini ni kama ifuatavyo:

 Inj. James Kilaba (Mwenyekiti), Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,
 Inj. Samson Mwela (Katibu), Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
 Prof. Idris Rai (Mjumbe), Makamu Mkuu wa Chuo, SUZA,
 Bi. Joan Mbuya (Mjumbe), Mkurugenzi wa Sera na Mipango-Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali,
 Inj. George Mulamula (Mjumbe), Mkurugenzi Mtendaji-DTBi,
 Bw. Juma Rajabu, (Mjumbe), Mkurugenzi Mtendaji-Maxcom Africa,
 Bw. Maharage Chande, (Mjumbe), Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Ofisi ya Rais-President’s Delivery Bureau, na
 Bw. Nicolaus Mhonyiwa (Mjumbe), Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA-Ofisi ya Msajili wa HAZINA.

Aidha, Tume ya TEHAMA inatarajiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na yafuatayo: Kushiriki katika kushauri juu ya uwekezaji wa TEHAMA nchini kwa ubia na sekta binafsi; kuwatambua, kujenga uwezo na kuwaendeleza wataalam wa TEHAMA; kushauri na kushiriki pamoja na wadau katika tafiti za TEHAMA, uwekaji viwango na ubunifu katika sekta ya TEHAMA; na kushiriki katika kusimamia miundombinu na programu za kitaifa za TEHAMA.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Eng. Maria Sasabo, alisisitiza kuwa Kamati ina kazi kubwa ya kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha kuwa Tume itatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na masuala ya uwekezaji; na kusimamia vema viwango vya wataalamu wa Sekta. Naye Mwenyekiti, Inj. James Kilaba, kwa niaba ya Kamati alishukuru kwa kuaminiwa na Serikali na pia aliahidi kuwa watatekeleza majukumu yao kikamilifu. Pia alimalizia kwa kusema, “hatutawaangusha”.

MWISHO
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali