UONGOZI wa Kampuni ya Lugumi Enterprises ambao umekuwa ukituhumiwa kupokea asilimia 99 ya malipo ya fedha toka Jeshi la Polisi Tanzania kwa tenda ya kufunga mashine maalumu za utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vyote vya Polisi Wilaya, leo umelazimika kuingia mitini na kuwaacha wanahabari solemba. Awali viongozi hao walitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwamba wangejitokeza kuzungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma zinazoelekezwa kwao.
Uongozi huo ulitoa taarifa kuwa ungezungumza na wanahabari katika mgahawa wa City Sport Lounge uliopo katikati ya jiji la Dar es Salaam majira ya saa tano na saa sita. Baada waandishi wa habari kufika eneo la tukio mapema walisubiri bila mafanikio na baadaye ilikuja taarifa kuwa wameshindwa kufika kuzungumza na wanahabari kwa kuwa wameitwa mjini Dodoma (Bungeni) kwenda kujieleza. Mtoa taarifa huyo alifika na nakala ya taarifa na kuigawa kwa wanahabari akidai iliandaliwa na uongozi wa Lugumu kuzungumza na wanahabari.
Taarifa hiyo ya kurasa mbili ambayo ilionekana imesainiwa na Juma Moshy Sabury kutoka Lugumi inabainisha kuwa ni kweli kwamba kampuni hiyo iliingia mkataba na Jeshi la Polisi wa kufunga mitambo ya utambuzi wa vidole katika vituo vya Polisi. Taarifa hiyo inasema makubaliano na Jeshi la Polisi ni kufunga vituo vya polisi Tanzania Bara na Visiwani kwa maelekezo ya jeshi hilo na kazi inaendelea.
Taarifa inasema hakuna matatizo kati ya pande zote za wabia wa mkataba yaani Jeshi la Polisi wala Kampuni ya Lugumi iliyolalamika juu ya mkataba huo, hali ambayo inaashiria utekelezwaji umefanywa vizuri. “…Kwa mujibu wa Mkataba, kama kuna mgogoro katika mkataba, upande usioridhishwa na utekelezwaji wake, utatangaza mgogoro kwa Mwanasheria Mkuu. Si Jeshi la Polisi kwa upande mmoja wala sisi kwa upande mwingine aliyetangaza mgogoro wowote dhidi ya mwingine, kwa mujibu na matakwa ya mkataba,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliwaomba wananchi kupuuza habari zinazotolewa na vyombo vya habari juu ya Lugumi kuwa hazina ukweli wowote.
Hivi karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ililiomba Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba ilioingia na kampuni ya Lugumi Enterprises wa kufunga mashine maalumu za kuchukua alama za vidole katika vituo vyote vya Polisi Wilaya, ili kujiridhisha na utekelezaji wa mkataba huo kutokana na kuwa na utata.
PAC ililazimika kuomba mkataba huo baada ya kubaini Jeshi la Polisi limeshailipa Kampuni ya Lugumi Enterprises kiasi kikubwa (asilimia 99) cha fedha ilhali kazi hiyo imefanywa katika vituo 14 tu vya Jeshi la Polisi kati ya vituo 108 vinavyostahili kufungwa mashine hizo.
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshy Hilal mara baada ya kupitia na kujadili taarifa ya Jeshi hilo alisema wameliagiza Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba huo, kujiridhisha zaidi kwani licha ya kazi hiyo kufanyika kidogo tayari Jeshi la Polisi lilikuwa limelipa asilimia 99 ya malipo yote ya mkatama mzima ambapo ni Shilingi bilioni 34 bila kodi.