Rais Dk Magufuli Amtumbua Hadharani Mkurugenzi wa Jiji Dar

Bw. Wilson Kabwe

Bw. Wilson Kabwe

Na Mwandishi Wetu, Dar

RAIS wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi hadharani Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Wilson Kabwe kwa kile kutuhumiwa kulisababishia Jiji hasara ya takribani shilingi bilioni 3 kutokana na kuridhia kuongezwa muda kwa mkataba wa tozo za mabasi ya mikoani katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani, Ubungo.

Rais Magufuli amelazimika kuchukua hatua hiyo leo alipokuwa akizinduwa Daraja la Kigamboni baada ya Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kueleza tuhuma za Wilson Kabwe mbele ya Rais alipopewa nafasi ya kuzungumza. Mkuu wa Mkoa Makonda alisema aliunda Kamati maalumu ya uchunguzi iliyofichua madudu na harufu ya ufisadi katika utekelezwaji wa mikataba mitatu, inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato ya Stendi Kuu ya Mabasi ya Mikoani ya Ubungo na kodi ya uegeshaji magari katikati ya mji.

“Kamati ile imebaini kuwa pale ubungo kunatumika sheria ndogo mbili za ukusanyaji mapato moja ya mwaka 2004 na nyingine mwaka 2009 kwa lengo la kunufaisha wachache, Lakini cha kushangaza tumebaini kuwa bado kampuni inayokusanya mapato katika kituo cha Ubungo, inawasilisha mapato hayo kwa kutumia sheria ya mwaka 2004 yaani Sh milioni 42 badala ya Sh milioni 82 kwa mwezi…”

“…Mbaya zaidi kamati ile katika ukaguzi wake, ilikuta kampuni ya ukusanyaji mapato hayo stendi ya Ubungo inayo Sheria ya Mwaka 2009 lakini katika nyaraka za Halmashauri ya Jiji zinaonesha sheria inayotumika ni ya mwaka 2004,” alisema Makonda.

Alifafanua kuwa Sheria Ndogo ya Mwaka 2004 ya ukusanyaji mapato ndani ya kituo hicho, inaonesha kuwa kila basi linatakiwa kutozwa Sh 4,000, hivyo makusanyo halisi kwa mwezi ni Sh milioni 42 kutokana na mabasi 350 yanayoegeshwa kituoni hapo. Hata hivyo, alisema kutokana na mabadiliko ya tozo, sheria hiyo ilibadilishwa mwaka 2009 na kila basi likawa linatozwa Sh 8,000 na hivyo makusanyo ya mwezi yakapanda na kufikia Sh milioni 82 kwa mwezi.

Baada ya ufafanuzi huo Rais Dk. Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi, Bw. Wilson Kabwe wakati taratibu zingine zikifanywa. Alimwelekeza Mkuu wa Mkoa Makonda suala la maelekezo kwa mikataba iliyosainiwa kinyume cha utaratibu ipo chini yake hivyo anaweza kutoa maelekezo stahili kwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji atakayekuja kuhusiana na mikata hiyo.

Rais Magufuli alisema amekula kiapo cha kuisimamia sheria hivyo atatekeleza hivyo siku zote bila kumuonea mtu kwani wananchi wameumia kwa muda mrefu sasa umefika muda wao wa kufuraia na viongozi nao waumie.

Hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar Makonda alisema baada ya kuunda kamati maalumu ya kufuatilia malalamiko ya muda mrefu, ambayo ofisi yake ilikuwa ikipokea kutoka kwa wananchi na kubaini madudu ya watendaji, alitangaza wazi kuwa hataki kufanya kazi na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Kabwe na Kaimu wake, Sarah Yohana na kuwasilisha majina yao kwa mamlaka husika ya nidhamu kwa hatua zaidi.

Alisema kwa mujibu wa uchunguzi, kamati hiyo ilibaini kuwa katika stendi ya mabasi ya Ubungo, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, ikiwemo kutokuwasilishwa kwa mapato halisi yanayotokana na makusanyo ya kila siku serikalini.