Ajali ya meli: Miili saba yapatikana Mombasa

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd

Zanzibar

MIILI ya watu saba waliokufa kwenye ajali ya meli ya Mv Spice Islanders imepatikana katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, Mombasa huko Kenya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd alithibitisha taarifa za kupatikana kwa miili hiyo jana wakati akipokea rambirambi kutoka kwa taasisi mbalimbali ofisini kwake Vuga, mjini hapa.

Alisema watu watano waliokotwa na kufanyiwa mazishi kwa taratibu zote za kidini katika Bahari ya Hindi huko Mombasa. Alisema taarifa hizo walizipata kutoka kwa Balozi mdogo wa Zanzibar huko Mombasa, Yahya Haji Jecha.

Alisema kutokana na taarifa hizo, kuna dalili kubwa za kupatikana kwa maiti wengine hivyo akatoa wito kwa wasamaria wema kuendelea kusaidia waathirika akisema misaada yao itatumika katika harakati za kutafuta miili iliyobaki na sehemu nyingine kwa ajili ya huduma kwa jamii ambazo zimeathirika.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed alisema jana kwamba miili miwili miili miwili ukiwamo wa kichanga kimoja imepatikana huko Tanga.

Wajitokeza kudai fidia

Mamia ya watu walionusurika katika ajali ya meli hiyo wameanza kumiminika katika ofisi za meli hiyo kudai fidia ya mali zao zilizo potelea baharini.

Baadhi ya watu hao walisema jana kwamba mpaka sasa hawafahamu kinachoendelea juu ya mali zao na wala hawajaonana na uongozi wa kampuni hiyo kupewa maelezo yoyote.

Miongoni mwa waathirika wa ajali hiyo, Ramadhan Khamis Haji alisema: “Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuninusuru na kifo lakini pia ninawaombea marehemu wote waliofariki katika ajali hiyo. Lakini nimebaki maskini kwani mali zangu zimepotea katika ajali hiyo.”

Alisema alikuwa ni mfanyabiashara wa bidhaa za umeme na kwamba alitoka mjini Unguja kununua bidhaa hizo kwa ajili ya kwenda kuziuza Pemba lakini mpaka sasa yeye na wenzake hawajui kinachoendelea na kila wakienda katika ofisi hizo hawaelezwi chochote.

Hata hivyo uongozi wa kampuni hiyo kupitia kwa ofisa mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Kapteni Mabruk alikataa kuzungumzia suala la madai ya manusura wa ajali hiyo.

“Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu bado liko mikononi mwa kamati iliyoteuliwa na Serikali kuchunguza chanzo cha ajali na mpaka hivi sasa tunapoongea wajumbe wa kamati hiyo wametoka hapa ofisini sasa hivi na kuchukua baadhi ya viongozi kwa mahojiano zaidi, hivyo mkitaka chochote kinachohusiana na suala la ajali ya meli hiyo nendeni serikalini,” alisema Kapteni Mabruk.

Simanzi Pemba

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Shariff Hamad jana alifanya ziara na kutoa pole kwa familia za wafiwa.

Katika viunga vya kisiwa cha Pemba, simanzi ilitanda katika ziara ya Seif aambaye alipita kutoa mkono wa pole kwa wananchi waliofiwa na ndugu zao katika ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia Jumamosi.

Maalim Seif aliwatembelea wananchi wa Pemba ikiwa ni siku moja tangu kufanyika hitima ya kuwaombea marehemu wa ajali hiyo, iliyohudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.

Akizungumza na ndugu waliofiwa katika ajali hiyo katika Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba, Maalim Seif alisema Serikali imeguswa na msiba huo na kwamba itashirikiana bega kwa bega na wananchi katika wakati huu mgumu.

“Tangu tukio hili, naweza kusema Serikali imejitahidi, lakini jitihada haishindi kudura. Bado jitihada za kuwatafuta wengine zinaendelea. Wenzetu kutoka Afrika Kusini wameleta wataalamu wapiga mbizi tangu juzi na sasa wameanza kazi,” alisema Maalim Seif.

Aliwashukuru wana kijiji wa Nungwi waliojitokeza baada ya meli kuzama na kutoa msaada kwa waathirika wa ajali.

“Wenzetu kutoka Nungwi tunawashukuru sana, walipopata taarifa tu, kila mmoja mwenye chombo chake alitoka kutafuta watu. Tunavishukuru pia vyombo vya ulinzi na hata wenye mahoteli,” alisema.

Katika Mkoa wa Kusini peke yake ambako Maalim Seif alianzia ziara yake, familia 194 zilizopoteza ndugu na jamaa zao.

Katika mitaa ya Mji wa Chake chake, watu walikaa kwa makundi wakisimuliana kuhusu tukio hilo, huku wengine wakifarijiana lakini wengi wakifuatilia taarifa za ndugu na jamaa zao wanaorudi kutoka Unguja baada ya kuokolewa katika meli hiyo.

Katika Uwanja wa Ndege wa Karume, Chakechake na Bandari ya Mkoani katika Mkoa wa Kusini Pemba, watu wengi walikuwa wakifuatilia kuwapokea au kupata taarifa za ndugu zao waliokuwa wamenusurika baada ya kuokolewa katika ajali hiyo.

Ushuhuda mwingine wa walionusurika
Mmoja wa walionusurika katika ajali hiyo, Salim Mohammed Rashid jana mjini Chakechake kwamba anaamini ya kuwa watu waliopotelea majini ni wengi kuliko maiti waliopatikana.

“Mimi niliokolewa saa nne asubuhi, tangu ajali ilipotokea saa saba usiku. Tulikutwa wawili tukiwa mbali mno na ajali. Kama siyo kuokolewa, tungepotea kabisa,” alisema Rashid.

Rashid ambaye ni mfanyabiashara, alisema amepoteza mzigo wake wa nyanya wenye thamani ya Sh5 milioni aliununua Makambako mkoani Iringa.

Rashid alielekeza shutuma zake kwa Mamlaka ya Bandari Zanzibar kwa kuzembea kuchukua hatua mapema licha ya wao kuwatahadharisha kabla meli haijaondoka.

“Kabla hata meli haijaanza safari, tulipiga kelele kwa watu wa bandari. Tulisema kuwa nyie mnataka kutuua, lakini wakanyamaza kimya. Tayari meli ilikuwa imelalia upande wa kulia. Mabaharia wakatuambia kuwa itakaa sawa tu.”

“Ilipofika saa saba usiku, tukasikia kelele kutoka nyuma ya meli, ‘tunakufa, tunakufaa’. Kwenda kuangalia, kumbe meli ilishajaa maji. Nahodha akatangaza kuwa wote tusiwe na wasiwasi, ila tuhamie upande wa kushoto. Hata tulipohamia, tulikuwa tumeshachelewa, meli ikaanza kuzama. Watu wengi tukajitupa majini, hapo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuiona meli.”

Mkazi mwingine wa Wete, Pemba, Juma Saleh Juma alisema amepoteza watoto sita aliokuwa akisafiri nao… “Unajua sisi tuna desturi ya kwenda kusherehekea Sikukuu ya Eid kwa ndugu zetu. Skuli (shule) zilikuwa zimefungwa, kwa hiyo nilisafiri na watoto wangu na wa ndugu zangu kwenda kula sikukuu. Sasa wakati tunarudi ndiyo yametukuta. Ajali ilipotokea sikuwaona tena, hadi nilipokuja kuokolewa.”

Katika hatua nyingine; Wadau mbalimbali wameendelea kutoa rambirambi zao kutokana na ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea katika visiwa vya Unguja na Pemba. Miongoni mwa waliotoa rambirambi zao ni Bunge la Afrika Mashariki ambalo limetoa Sh2 milioni na Baraza la Wakilishi lililotoa Sh15 milioni.
CHANZO; Mwananchi