PAC Yanusa ‘Madudu’ ya Jeshi la Polisi…!

IGP, Ernest Mangu

IGP, Ernest Mangu

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imelitaka Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba ilioingia na kampuni ya Lugumi Enterprises wa kufunga mashine maalumu za kuchukua alama za vidole katika vituo vyote vya Polisi Wilaya.

PAC imelazimika kuomba mkataba huo baada ya kubaini Jeshi la Polisi limeshailipa Kampuni ya Lugumi Enterprises kiasi kikubwa cha fedha ilhali kazi hiyo imefanywa katika vituo 14 tu vya Jeshi la Polisi kati ya 108 vinavyostahili kufungwa mashine hizo.

Akizungumza Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshy Hilal mara baada ya kupitia na kujadili taarifa ya Jeshi hilo alisema wameliagiza POlisi kuwasilisha mkataba huo Aprili 11, kujiridhisha zaidi kwani licha ya kazi hiyo kufanyika kidogo tayari Jeshi la Polisi limelipa asilimia 99 ya malipo yote ya mkatama mzima ambapo ni Shilingi bilioni 34 bila kodi.

Wakati huo huo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limeiomba kamati hiyo kuruhusiwa kuagiza bidhaa zao wenyewe katika maduka ya Jeshi kwani bei ambazo waagizaji huwauzia bidhaa hizo mara baada ya kuagiza hazina tofauti na zile za kawaida ilhali waagizaji hao hufutiwa kodi kutokana na bidhaa wanazoingiza.

Bw. Hilal ambaye ni Mbunge wa sumbawanga Mjini alisema watafikisha ombi la JWTZ bungeni ilikuangaliwa kwa kina. Alisema kampuni zinazoingiza bidhaa hizo kwa Jeshi hazilipi ushuru hivyo bidhaa wanazoziingiza kwa jeshi hazitakiwi kuwa na bei ya juu.