NAHODHA wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Benki ya NMB, Richard Mwalwiba amekabidhi rasmi vikombe vya ushindi wa Mashindano ya Ligi ya Mabenki ‘Brazuka Kibenki’ kwa Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi. Ineke Bussemaker ikiwa ni pamoja na kutoa shukrani kwa uongozi wa benki hiyo kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu yake.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, ambapo uongozi wa timu ya mpira wa miguu ya NMB ilipofanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya NMB kuelezea mafanikio na changamoto za mashindao hayo. Timu ya NMB ilifanikiwa kutwaa vikombe viwili katika ligi ya ‘Brazuka Kibenki’ iliyoshirikisha mabenki mbalimbali nchini Tanzania. NMB ilifanikiwa kutwaa kombe la ushindi wa tatu wa mashindano hayo pamoja na Kikombe cha Timu Bora iliyojipanga vizuri katika ushiriki wa mashindano hayo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vikombe hivyo, Nahodha Mwalwiba alisema timu yake ilifanikiwa kupata ushindi baada ya kujiandaa vizuri kimashindano ikiwa ni pamoja na nidhamu kwa wachezaji na kuzingatia mazoezi na maelekezo ya Kocha wa timu, Mohamed Hussein (Machinga) ambaye ni nyota wa zamani wa mpira wa miguu nchini.
Alisema kikosi chake mbali na kufanikiwa vikombe hivyo pamoja na medali za shaba pia kilifanikiwa kutoa Mchezaji Bora wa Mashindano na mfungaji bora, Ahmed Nasoro pamoja na kutoa wachezaji bora watatu walioenda kuunda kikosi kimoja cha timu ya mabenki. Alishauri mashindano yajayo timu za mabenki kuzingatia kanuni za mashindano na kuacha kuchezesha wachezaji ambao hawana sifa ili ligi kuleta msisimuko zaidi.
Kwa upande wake Meneja wa Timu ya NMB, Bi. Josephine Kulwa alisema ili kujiweka vizuri katika mashindano yajayo tayari wachezaji wote wa NMB wameanza mazoezi ya aina mbalimbali chini ya wakufunzi wa mazoezi. “…Sisi tupo fiti muda wote kimichezo, tunavyozungumza hivi sasa tayari wachezaji wanafanya mazoezi yote kujiweka vizuri zaidi,” alisema Bi. Kulwa.