Prof. Mbarawa Akagua Barabara Tabora-Koga-Mpanda
WAZIRI WA UJENZI, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza mradi wa ujenzi wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa Km. 356 kwa kiwango cha lami ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano aliyoitoa kwa wananchi wa Mikoa ya Katavi na Tabora.
Ametoa kauli hiyo wilayani Sikonge mkoani Tabora, mara baada ya kukagua barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amesema ujenzi huo unatarajia kuanza rasmi hivi karibuni.
‘Ujenzi wa barabara hii tumeugawa katika sehemu tatu ili kuharakisha utekelezaji wake, tutahakikisha ifikapo mwisho wa mwaka huu, makandarasi wote watatu watakuwa katika maeneo yao ya kazi’, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza kuwa wananchi wanaostahili kulipwa fidia watalipwa kwa wakati kwa kuwa takribani shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Prof. Mbarawa pia amekagua daraja la Koga linalounganisha Mkoa wa Katavi na Tabora na kuwataka viongozi wa mikoa hiyo kuhakikisha kuwa magari yasiyozidi tani tatu ndio yanayopita katika daraja hilo ili kuepusha ajali hadi ukarabati mkubwa utakapofanyika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Kanali Mstaafu Issa Nziku amemuomba Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupandisha hadhi baadhi ya barabara katika Wilaya hiyo ili zihudumiwe na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutokana na uwezo mdogo wa Halmashauri hiyo kuzikarabati kila wakati.
Katika Hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua uwanja wa Ndege wa Tabora na kuwataka viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) kuangalia namna bora ya ukarabati wa kiwanja hicho ili uruhusu ndege kubwa kutua na kuongeza biashara.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku saba ya kukagua miundombinu ya taasisi zilizo chini ya Wizara yake katika mikoa ya Magharibi ili kuifungua kanda hiyo kimiundombinu na hivyo kufufua fursa za kiuchumi.