Serikali ya Uingereza imeanzisha uchunguzi wa dharura kufuatia ufichuzi kuwa wachezaji nyota wa kandanda nchini Uingereza wamekuwa wakitumia madawa yaliyopigwa marufuku ya kuongeza nguvu mwilini.
Gazeti la Sunday Times limechapisha ripoti ya uchunguzi iliyothibitisha kuwa sio tu wasakataji dimba bali hata waendesha baiskeli, wachezaji Kriketi na hata wachezaji wa tenisi wamekuwa wakipokea matibabu kutoka kwa daktari mmoja ambaye anajulikana kwa kupeana madawa hayo yaliyopigwa marufuku ya kututumua misuli.
Daktari Mark Bonar ambaye anazahanati yake mjini London Uingereza amekuwa akiwatoza wachezaji nyota maelfu ya pauni za Uingereza kwa matibabu hayo fiche ambayo imegunduliwa kuwa ni matibabu ya madawa yaliyopigwa marufuku na shirikisho la kupambana na madawa haramu WADA.
Wateja wakuu wa Dkt Bonar yasemekana ni wachezaji wa timu kuu katika ligi maarufu zaidi duniani ligi ya Uingereza.
Uchunguzi pia umebaini kuwa dkt Bonar amekuwa akiwapa wachezaji nyota 150 dawa aina ya EPO Steroids na hata homoni zinazokua kwa
haraka ambazo ni haramu katika michezo katika kipindi cha miaka 6 sasa.
Serikali ya Uingereza imeanzisha uchunguzi dhidi ya taasisi ya kupambana na kuenea kwa madawa hayo haramu kufuatia ufichuzi huo.
Hakuna ushahidi kuwa timu za ligi kuu ya Uingereza zilifahamu mbinu za dkt Bonar.
Aidha Sunday Times linasema kuwa halina ushahidi ‘huru’ kuwa dkt Bonar aliwapa madawa hayo ya kututumua misuli wachezaji wangapi wanaochezea vilabu vya ligi kuu ya Uingereza EPL.
Hata hivyo wachezaji kadhaa walioulizwa iwapo walipewa madawa hayo ya kututumua misuli na dkt Bonar walikataa kujibu na wengine wakakanusha madai hayo ya daktari huyo.
Dkt Bonar hata hivyo anasema kuwa hakuwapa wachezaji hao madawa hayo kwa nia ya kuimarisha uwezo wao uwanjani ila anadai aliwapa madawa hayo ilikuwatibu dhidi ya maradhi mbali mbali waliokuwa wanaugua.
Uchunguzi huu unatokana na ufichuzi wa mchezaji mmoja aliyekwenda kwa idara ya serikali kumshtaki dkt Bonar kwa kumpa dawa iliyopigwa marufuku.
Mchezaji huyo ambaye ametaka jina lake libanwe anasema alipigwa na butwaa dkt Bonar aliposisitiza kuwa anastahili kumeza dawa hiyo haramu.
Sunday Times lilitumia mwanariadha chipukizi kumrekodi daktari huyo akijigamba jinsi alivyowatibu wachezaji wengi tu nyota akitumia mbinu zizo hizo japo ni marufuku.
Chanzo:BBC Swahili