Na HakiElimu
JIULIZE, kati ya mwanaume na mwanamke aliyesoma; ni nani huwakumbuka wazazi wake zaidi? Ni nani hajali watoto na familia yake zaidi? Ni nani hurudi kijiji kwao mara kwa mara? Ni nani mwaminifu wa kipato chake? Ni nani hujali afya ya uzazi na malezi zaidi?
Majibu ya maswali haya ndiyo sehemu ya mjadala wa leo kuhusu faida za kusomesha wasichana/wanawake. Endelea……
Wasichana wakielimika wanakuza uwezo mkubwa wa kufikiri kwa umakini na uyakinifu. Uwezo huu ndio unaohitajika sana katika jamii ya leo. Mtu mwenye uwezo wa kufikiri ndiye mwenye nguvu ya kuibua dhana mpya, kutafuta njia mbadala za kutatua matatizo na kuelekeza wenzake katika matendo sahihi. Uwezo wa kufikiri ndio unaomuongoza mtu kila siku katika utendaji wake.
Wanawake wenye elimu ndiyo wanaojitambua na kujimiliki wenyewe kwanza, kuzikabili changamoto zinazowasonga, kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayowazunguka ili kuboresha maisha yao.
Wanawake wakisoma wanapata uwezo wa kujitambua na kujiamini. Kujitambua huko kunaendana na uwezo wa mtu kujua haki zake na wajibu wake katika jamii. Kujiamini katika kutoa uamuzi na kushiriki katika masuala yote ya kiuchumi kisiasa na kijamii. Wataweza kujiamulia mambo yao wenyewe na kujitawala.
Wanapata uwezo wa kutumia fursa zilizopo na kutengeneza fursa ili kujiletea maendeleo. Kwa mfano, kupata fursa ya kuajiriwa na kujiajiri wenyewe kutokana na maarifa na ujuzi walioupata.
Maarifa ndiyo yanayowaongoza kutumia fursa zilizopo kama vile ardhi, madini, misitu, kubuni biashara na nyinginezo. Bila elimu, wanawake hawawezi kupata fursa nyingi wala kuzitumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo yao na ya jamii.
Wanawake waliosoma hukumbuka wazazi na familia zao zaidi kuliko wanaume. Hurudi nyumbani muda wote na kuwatunza wazazi kwa ukamilifu. Wanaume waliosoma wengi hupotelea mijini na nje ya nchi kwa miaka kadhaa, bila kurudi nyumbani wala kukumbuka wazazi na familia. Wanawake waliosoma hawafanyi hivyo.
Wanawake waliosoma huzaa watoto wachache na kujenga familia ndogo zenye afya, elimu na zenye ustawi bora. Kwa mujibu wa utafiti wa bwana Raney, mwanamke aliyesoma ana wastani wa kuzaa watoto wawili hadi watatu, ambao anaweza kuwahudumia kikamilifu.
Lakini, mwanamke asiyesoma ana wastani wa kuzaa watoto sita mpaka saba ambao wengi wao wanashindwa kuwahudumia vyema. (Subbarao & Raney 1995). Fanya utafiti kwenye familia yako kuthibitisha hili.
Kumsomesha mwanamke, kunachangia kwa asilimia kubwa kuokoa uhai wa watoto wengi, kupunguza utapiamlo na kupunguza vifo vya watoto kwa asilimia tano hadi 10. Mwanamke aliyesoma atakuwa mama wa watoto anayejua kanuni za afya, lishe bora ya mtoto na uzazi bora. Hivyo, atailinda afya ya familia yake dhidi ya maradhi.
Pia utafiti unaonyesha kwamba, watoto wanaozaliwa na mama wenye elimu nzuri, wana uwezekano wa zaidi ya asilimia 70 kufaulu masomo na kufanikiwa kielimu (Uwezo 2010). Pia ukiongeza uandikishaji wa wasichana shuleni kwa asilimia kumi tu, unakuwa umepunguza vifo vya watoto wanne kati ya 1000.
Tena mwanamke aliyesoma ana uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto akiwa tayari amepevuka. Na sio katika umri mdogo. (Schultz 1993). Kwa faida kama hizi kwa nini tusisomeshe watoto wa kike wote?
Pia tafiti zinaonyesha wanawake waliosoma wana asilimia kubwa ya kukwepa maambukizi ya Ukimwi na kuishi kwa muda mrefu. Maana wanapata taarifa zaidi kuhusu ugonjwa huo.
Wanakuwa wanafahamu njia za kujikinga, wanakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kuhusu miili yao na juu ya uhusiano wao na wanaume. Wanawake wasiosoma wana hatari ya kuambukizwa Ukimwi kwa asilimia kubwa kuliko wanawake waliopata elimu. (Delamonica, 2000).
Kuwasomesha wanawake kunachangia ongezeko kubwa la pato la taifa na uzalishaji katika kilimo hasa kwa nchi zinazotegemea kilimo kama Tanzania. Tafiti zinaonyesha mwanamke aliyesoma na kupata elimu, uzalishaji wake huongezeka na pia hupunguza utapiamlo katika familia kwa asilimia 43 (Lisa & Haddad, 1995).
Wanawake waliosoma wana uwezo mkubwa wa kufanya uamuzi sahihi wenye mantiki na tija. Wasio soma hushindwa kufanya uamuzi wenye tija. Kwa mfano, wasichana wengi wasio na elimu wanashindwa kulinda miili yao na hadhi yao.
Wengi wanatumiwa kama vyombo vya starehe na wanaume wasio na hekima. Na hata kipindi cha uchaguzi, wanawake wasiosoma ndio wanaotumiwa kuwaingiza madarakani mafisadi na wahujumu uchumi wa nchi. Wanapiga kura bila kujitambua!
Mwisho, wanawake wakipata elimu ni vigumu sana kwao kuendeleza mila potofu kama kukeketa watoto wao au kuwaoza watoto wao wakiwa wadogo.
Ni vigumu kwa wanawake waliosoma kunyanyaswa na wanaume katika jamii na taasisi zinazoendeleza mfumo dume na ukandamizaji wa wanawake. Watajua haki zao na kuzilinda. Na watachangia zaidi maendeleo ya jamii. Kwa faida hizi kwa nini tusisomeshe watoto wa kike? Ni Falsafa Mbadala!
Imeandikwa Na Mtemi Zombwe anapatikana kupitia 0713-000027