Arusha watakiwa kutenga maeneo ya wazi

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye

Na Janeth Mushi, Arusha

UONGOZI wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na idara ya ardhi wametakiwa kutenga maeneo ya huduma za kijamii ikiwemo sekta ya elimu wakati wanapogawa ardhi katika maeneo mapya.

Changamoto hiyo imetolewa juzi mjini hapa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye alipokuwa akihudhuria hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujeni wa shule ya sekondari ya kata (Sokoni II). Medeye alisema katika halmashauri anuai nchini Maofisa wa Ardhi wamekuwa wakigawa maeneo mapya ya makazi kwa kugawa eneo zima bila kujali sehemu za huduma za kijamii zitakazotumiwa na wananchi.

“Idara za ardhi katika halmashauri zinatakiwa kuhakikisha kuwa wakati wanagawa maeneo mapya kwa ajili ya makazi ni muhimu kutenga maeneo ya huduma za kijamii ikiwemo shule na hospitali,”

Aidha hali ya kata kutokuwa na shule ya sekondari inawasababisha wanafunzi wanaoishi katika kata hiyo kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata masomo katika kata nyingine za jirani.

Aliwataka wananchi kujikita zaidi katika kuchangia sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule kwani urithi pekee kwa watoto ni elimu ambayo itawawezesha kushindana na soko la ajira ambalo linakuwa siku hadi siku.

Kwa mujibu wa Ole Medeye alisema kuwa ni vizuri halmashauri zinapogawa maeneo mapya zikawafidia wananchi wanaoishi jirani na shule za kata ili kupisha upanuzi wa shule hizo kwani shule nyingi za kata zimetengewa maeneo finyu na kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi jambo ambalo uongozi wa shule unashindwa kupanua ujenzi wa shule.
Jumla ya sh. milioni 40 zilipatikana ambapo naibu Waziri huyo alichangia sh. milioni 5, huku ujenzi wa jengo la shule hiyo ukikadiriwa kugharimu milioni 540 hadi kukamilika.

Wachangiaji wengine alikuwa ni Mkurugenzi wa Monaban LTD, Philemon Mollel ambaye alichangia sh. milioni 5, huku mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa shule hiyo, Betuel Mbalakay ambaye alichangia sh. milioni 5.