SBL kufadhili masomo kwa wanafunzi wasiojiweza 2011

Mkurugenzi wa Mahusiano wa SBL, Teddy Mapunda.

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) imetangaza kuanza kwa mchakato wa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2011. Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 12 kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mahusiano wa SBL, Teddy Mapunda.

Kwa mujibu wa Bi. Mapunda amefafanua kuwa mpango huo wa ufadhili uko wazi kwa wanafunzi wenye uwezo kutoka ukanda mzima wa Afrika Mashariki wasio na uwezo, lakini wenye shauku ya kuendelea na masomo ya juu katika fani za Biashara, Teknolojia ya Habari, Uhandisi pamoja na Sayansi ya Vyakula.

Ufadhili huu unajumuisha gharama za ada ya masomo, vitabu, malazi, pesa ya kujikimu pamoja na mpango wa kazi kwa wanafunzi watakokuwa wamefanikiwa.

“Tunaelewa umuhimu wa elimu kwa jamii. Hatufanyi kazi ya kuwapatia watu uwezo pekee bali pia kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye pamoja na ya jamii zao,” ameeleza Mkurugenzi huyo wa Mahusiano wa SBL, Bi. Mapunda.

Mkurugenzi wa Mahusiano wa SBL, Teddy Mapunda (kulia) akiwa na Nandi Mwiyombella, CSR & RD Manager (SBL)


EABL Foundation imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Kitanzania tangu mwaka 2005 na hadi kufikia sasa wanafunzi 20 wamefaidika na mpango huu.

Kwa mwaka huu wa ufadhili, tunatarajia kusaili wanafunzi 10 na miongoni mwao, wanafunzi wanne watapata ufadhili kamili wa masomo ikiwa ni pamoja na tuisheni, malazi na baadhi ya pesa za kujikimu. Tayari tumewekeza kiasi cha shilingi milioni 140 kwa ajili ya mpango huu hapa Tanzania.

Wahusika watakuwa wanafunzi ambao tayari wameshapata barua za kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa shahada za biashara, uhandisi, sayansi ya chakula na shahada zinazohusiana na teknolojia ya mawasiliano.