Michuano ya Europa League imeendelea tena usiku wa kuamkia leo kwa michezo minane ambapo Liverpool wametinga robo fainali baada ya kutoka sare ya 1-1 na wenyeji, Manchester United katika Uwanja wa Old Trafford.
Manchester United walianza kuandika bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Anthony Martial dakika ya 32 kipindi cha kwanza ambao ulijaa wavuni.
Liverpool ikasawazisha bao hilo kupitia kwa Philippe Coutinho katika dakika ya 45 kipindi cha pili.
Hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika matokeo ikawa ni sare ya bao 1-1, lakini Liverpool ikisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 kufuatia ushindi wa mabao 2-0 ilioupata katika mchezo wa awali wakiwa ugenini.
Na katika matokeo mengine Tottenham nayo imeaga michuano hiyo baada ya kufungwa 2-1 na Borussia Dortmund, Mabao yote ya Dortmund yamefungwa na mwanasoka bora wa Afrika, Pierre-Emerick Aubameyang dakika ya 24 na 70, wakati bao la Spurs limefungwa na Heung-Min Son dakika ya 73.
Dortmund inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-1, baada ya wiki iliyopita kushinda 3-0 Ujerumani.
Sevilla imeifunga 3-0 FC Basel, mabao ya Adil Rami na Kevin Gameiro mawili Uwanja wa Ramon-Sanchez Pizjuan, hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-0 baada ya awali kutoa sare ya 0-0 ugenini.
Shakhtar Donetsk imeshinda ugenini 1-0 dhidi ya RSC Anderlecht, bao pekee la Eduardo Alves da Silva dakika za majeruhi Uwanja wa Constant Vanden Stockstadion, hivyo inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-1 baada ya awali kushinda 3-0 nyumbani.