Na Jacquiline Mrisho Maelezo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,TAMISEMI, George Simbachawene amewataka Wakuu wa Mikoa walioapishwa kufanya kazi kwa bidii na kutumia muda mwingi kutatua kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Simbachawene ameyasema hayo Jijini Dar es salaam alipokutana na Wakuu hao wa Mikoa ambapo amewasisitiza kwenda na kasi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili kutimiza malengo yaliyopangwa katika uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.
“Mfumo wa sasa wa uongozi ni tofauti na mfumo wa zamani, namna Mhe. Rais anavyotaka tufanye kazi ni tofauti na zama zingine zilizopita,Wakuu wa Mikoa mnapaswa kujua kila kinachoendelea kila siku katika Mikoa yenu na mnapaswa muwajibike kwa wananchi wenu”alisema Simbachawene.
Simbachawene ameongeza kuwa,Wakuu wa Mikoa wamepewa madaraka ya kusimamia mfumo wa ufanyaji kazi kwa kuhakikisha watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo kwakua nchi haiwezi kubadilika kama hakutakua na utendaji mzuri.
Aidha, Simbachawene amewakumbusha Wakuu wa Mikoa wazingatie na kusimamia haki za wananchi kwakua kuna baadhi ya mamlaka za Serikali za Mitaa zinaripotiwa kuwaonea sana wananchi hasa wanawake katika kupata haki zao maana ndio wanaongoza kwa kunyanyaswa.
Pia amewataka Wakuu wa Mikoa kutumia mamlaka waliyopewa kuvunja mabaraza yote ya usuluhishi yasiyozingatia sheria katika kutoa maamuzi na kuunda mabaraza mapya yenye sifa za kutatua kesi za wananchi.
Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,TAMISEMI, Mhe. Selemani Jaffo ameahidi kuwapa Wakuu wa Mikoa ushirikiano wa kutosha kutoka Ofisi ya TAMISEMI ili kuhakikisha kazi zao zinafanyika kwa ufanisi.