WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewahimiza wakazi wa Wilaya ya Mpanda ambayo inatarajiwa kuwa Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Katavi wachukue mikopo benki na kuwekeza kwenye majengo kukidhi mahitaji ya wilaya mpya.
Ametoa kauli hiyo Jumamosi, Septemba 10, 2011 akiwahutubia wakazi wa Mji wa Mpanda kwenye Uwanja wa Michezo wa Kashaulili, wilayani Mpanda, mkoani Rukwa. Amesema kuundwa kwa mkoa mpya wa Katavi kutakuja na changamoto kubwa ya kuwepo kwa mahitaji ya majengo kwa ajili ya makazi ya watumishi na majengo kwa ajili ya ofisi za baadhi ya taasisi.
“Kupata mkoa mpya na wilaya mpya ni fursa nzuri ambayo inakuja na changamoto zake. Nendeni mkakope na kujenga…patahitajika migahawa na nyumba za kulala wageni kwa ajili ya watalii watakaokuja mbuga ya Katavi na hasa uwanja wa ndege ukishakamilika na kuanza kazi,” alisisitiza.
Aliwaambia mamia ya wakazi hao kwamba kuna watu waliamua kuzusha maneno kuhusu uwekezaji katika wilaya ya Mpanda na hasa maeneo ya Katumba ambako kulikuwa na kambi za wakimbizi kutoka Rwanda.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa uwekezaji katika wilaya ya Mpanda ni wa lazima kama kweli wakazi wake wanataka kuondokana na umaskini kwani maeneo mengine wamepiga hatua za maendeleo kupitia njia hiyo hiyo ya uwekezaji.
“Ndugu zangu wana Mpanda njia pekee ya kututoa hapa tulipo ni kupitia uwekezaji kama ambavyo mikoa mingine imefanya na ikaweza kusonga mbele kimaendeleo… tunahitaji wawekezaji wa ndani na wa nje katika kuleta maendeleo,” alisema.
“Hili suala la Katumba ni kama nilijipalia makaa lakini ni lazima niseme kuwa nililifanya kwa nia njema… Katumba si eneo la kijiji hata kidogo. Hakuna mwanakijiji amefukuzwa pale ili kumpisha mwekezaji. Ni msitu wa Serikali ambao ulitolewa ili wakimbiz wake pale.”
“Baada ya wakimbizi kuondoka tukajiuliza lile eneo tunalifanya nini: libaki na kurudi kuwa msitu au tunafanya nini? Tulipata wawekezaji wa kujenga chuo, lakini tatizo likawa ni umbali tukajiuliza ni nani ataenda kusima kule wakati hakuna umeme wala barabara?”
“Tulipobaini kuwa hapatafaa kuweka chuo, tukaona tutafute wawekezaji katika kilimo ambao watakuja kufungua viwanda na kuwasadia wanavijiji wa maeneo ya jirani. Hawa wanaopiga kelele kama nia yao ni kutaka eneo la Katumba, waje basi waseme wana mtaji kiasi fulani nasi tunataka kuwekeza,” alifafanua.
Mbali ya maeneo ya Katumba kulikokuwa na kambi ya wakimbizi, Waziri Mkuu aliyataja maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo kuwa ni mapori yaliyoko njia ya kutoka Mpanda hadi Karema, Mpanda hadi Mwese na Urwila hadi Sikonge.
Alisema haina maana kuyaacha mapori hayo yakae tu wakati hakuna mkazi wa wilaya hiyo mwenye uwezo wa kuwekeza katika kilimo kikubwa. “Fanyeni kazi kwa bidii, acheni maneno maneno huku mkiendelea kulalamika njaa,” aliongeza.
“Leo tumepata benki hapa Mpanda, nimemuuliza Mwenyekiti wa wakulima wa tmbaku wilayani Mpanda, mheshimiwa Kakoswe kuwa mambo yakoje kwa wakulima wangu wa tumbaku akasema wana uhakika wa kupata sh. bilioni 32 baada ya kutoa mkopo wa benki wa sh. bilioni 10/- …hii si kazi ndogo.” Mhe. Kakoswe ni mbunge wa Mpanda Vijijini.
Alisema kama kila mmoja atafanya kazi kwa bidii, wilaya hiyo itaweza kusonga mbele lakini kama watabakia kuuza maneno tu, watakufa kwa njaa na watakwisha.
Waziri Mkuu pia alitoa vifaa vya muziki kwa vijana wa kundi la HipHop la mjini Mpanda kutokana na uimbaji wao wa nyimbo zenye ujumbe mzuri. Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea Dar es Salaam Septemba 11, 2011 mchana.