Rais Vietnam Aenda CCM Kuonana na JK

Rais wa Vietnam, Truong Tan Sang.

Rais wa Vietnam, Truong Tan Sang.

Na Beatrice Lyimo – Dar es salaam
 
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na  Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete leo amekutana na kufanya mazungumzo na  Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Truong Tan Sang katika ofisi ndogo za Makao makuu ya Chama cha Mapinduzi mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya mapokezi  ya Rais huyo, Dk. Kikwete amesema kuwa lengo la ujio wa Rais wa wa Vietnam katika ofisi za CCM ni kudumisha na kuendeleza uhusiano wa
kihistoria uliopo kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Komunisti cha Vietnam.
Amesema Chama cha cha Komunisti cha Vietnam na chama cha TANU na ASP vimekuwa  na mahusiano ya muda mrefu ya kihistoria toka kipindi ambacho vietnam ilikua ikipambana na ubeberu wa kimarekani.
Ameeleza kuwa katika mapambano hayo Chama cha TANU kiliunga mkono juhudi hizo kwa kuwaunga mkono wananchi wa Vietnam katika ukusanyaji wa michango mbalimbali iliyowezesha mapambano dhidi ya Ubeberu wa Kimarekani.
Aidha, amebainisha kuwa ujio wa Rais huyo wa Vietnam kama kiongozi wa Mkuu wa Chama na Serikali katika ofisi ndogo za Makao makuu ya CCM ni ishara ya kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya vyama hivyo viwili ambavyo viko madarakani.