Mkali na Bingwa wa ndondi Mfilipino ambaye ni mwanasiasa Manny Pacquiao amelitetea pigano lake lijalo na mwanamasumbwi Mmarekani Timothy Bradley dhidi ya madai kuwa litakiuka sheria za kampeni kabla ya uchaguzi unaokuja wa Mei
Tume ya Uchaguzi Ufilipino imepokea malalamishi kuwa pigano la Pacquiao mnamo Aprili 9, litakalorushwa nchini Ufilipino na kote ulimwenguni, litampa faida isiyo ya haki ya kupata umaarufu kupitia vyombo vya habari.
Walalamishi wanahoji kuwa pigano hilo linapaswa kuahirishwa hadi baada ya uchaguzi wa Mei 9. Hata hivyo mawakili wa Pacquiao mwenye umri wa miaka 37 wamejibu kuwa pigano hilo siyo “shughuli ya kisiasa inayoegemea upande wowote”
Wanasema nia yake ya kushiriki pigano hilo, ambalo huenda ikawa mara ya mwisho kwake kupanda ulingoni, hailengi kumpa faida yoyote isiyo ya haki. Badala yake ni kitu cha kuipa nchi na watu wake fahari na sifa wanayostahili, kabla ya bondia huyo kuumaliza ujana wake.
Pacquiao anakabiliwa na kibarua kikali cha kushinda kiti katika baraza la Seneti baada ya uchunguzi wa maoni kuonyesha kuwa alipoteza uungwaji mkono kufuatia matamshi yake ya kupinga ushoga aliyotoa kwenye televisheni moja nchini humo katikati ya mwezi uliopita.