Breaking News; Ajali juu ya ajali Zanzibar, hadi sasa 250 waokolewa kwenye ajali ya Meli ya Spice

Picha ya meli hiyo ikiwa imezama (Picha na Ahmed Muhamed Ahmad zanzinet)

TAARIFA ambazo zimetumwa na mmoja wa mashuda, kutokea Zanzibar, anasema ajali nyingine ya gari imetokea na watu watatu wamekufa papo hapo kati ya wananchi ambao wanaelekea eneo la Nungwi kuangalia ndugu zao waliopata ajali kwenye Meli ya Spice Islanders.

Na taarifa za sasa zinaeleza, watu 250 wameokolewa wakiwa hai katika meli iliyozama ya Mv Spice Islanders iliyokuwa ikitokea Bandari ya Malindi Unguja kuelekea Bandari ya Wete Kisiwani Pemba.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed amesema watu hao wameokolewa na Vikosi vya uokoaji na wananchi mbalimbali wanaotoa msaada wa uokozi katika tukio la kuzama kwa meli hiyo huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja. Waziri Aboud amesema watu hao wamesafirishwa kwa kutumia Boti zinazokwenda kasi za Zanzibar ambazo ilikwenda kutoa msaada katika eneo la tukio.

Amesema watu hao baada ya kufika Bandari ya Malindi Unguja watapelekwa Viwanja vya Maisara kwa ajili ya kuungana na familia na jamaa zao. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein yupo katika eneo la tukio huko Nungwi ili kujionea hali halisi ya tukio hilo.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kwa sasa Serikali inasafirisha maiti zote na majeruhi kuelekea Uwanja wa Maisara mjini, hivyo ndugu, jamaa na marafiki wasiendelee kwenda eneo la tukio Nungwi.