BOMU LA CHADEMA KWA PINDA HADHARANI.

SAKATA la vurugu na mauaji yaliyotokana na maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Arusha linaelekea kumuelemea Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Hiyo inatokana na taarifa ya kuwa kauli ya Waziri Mkuu Pinda ya wiki iliyopita iliyokituhumu CHADEMA kuhusika na vurugu hizo zilizoishia katika mauaji ya watu watatu, ilitokana na maoni ya Polisi ambao katika matukio hayo wao ni watuhumiwa.

Baada ya Pinda kutoa taarifa kuhusu tukio la Arusha bungeni, Mbunge wa Arusha Mjini kupitia CHADEMA, Godbless Lema, aliomba Mwongozo wa Spika, akitaka kujua mbunge anaweza kufanya nini akibaini ya kuwa “kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu analidanganya Taifa na Bunge ”.

Baada ya kuomba Mwongozo wa Spika, Spika Anne Makinda, alimtaka Lema kuwasilisha bungeni ushahidi wa “uongo wa Waziri Mkuu”, ifikapo juzi Jumatatu.

Hata hivyo ilipofika Jumatatu Spika Makinda aliliambia Bunge kwamba badala ya kuwasilisha bungeni, sasa Lema alitakiwa awasilishe utetezi wake kwa Spika mwenyewe kwa maandishi.

Habari za ndani na nje ya Bunge zinasema kwamba suala hilo la Lema na Waziri Mkuu Pinda limeibua makundi ambayo yameanzisha kampeni za siri zikilenga kuonyesha kuwa kwa kauli yake kuhusu vurugu na mauaji ya Arusha ambazo zilielemea utetezi wa Polisi pekee, yeye si mtu makini.

Taarifa za hakika zinasema tayari Lema amekwishakuwasilisha utetezi wake unaopingana na yale aliyoeleza Waziri Mkuu Pinda bungeni akianzia na taarifa ya kuwa waliofikwa na mauti katika vurugu na mauaji hayo ni Watanzania watatu kama alivyoeleza Waziri Mkuu Pinda ingawa ukweli ni kwamba waliofariki dunia ni Watanzania wawili, Dennis Michael Shirima na Ismail Omary, na Mkenya, Paul Njuguna.

Hoja nyingine katika utetezi wa Lema inaelezwa ni juu ya utaratibu wa maandamano ya Arusha kama alivyoeleza Waziri Mkuu Pinda kwamba Jeshi la Polisi lilipendekeza njia moja ya maandamano itumike lakini  viongozi wa CHADEMA walikataa.

Katika utetezi wake Lema anadai kwamba si kweli kwamba Polisi walielekeza hivyo, na kwa mujibu wa  nyaraka ambazo Raia Mwema imafanikiwa kuona, Lema anasema si kweli pia kwamba waandamanaji walikaribia mita 50 kutoka Kituo cha Polisi ambako ndiko kulikozuka mauaji yale kwa vile CHADEMA kina ushahidi wa picha za video zinazoonyesha ya kuwa mmoja wa waliouawa alifikwa na mauti eneo la mbali na Kituo cha Kati cha Polisi.

“Kama ni kweli hatua zote zilichukuliwa na Jeshi la Polisi basi ni wazi kwamba watu waliouawa au kujeruhiwa waliuawa au kujeruhiwa kwenye uzio au mlango wa Kituo cha Kati cha Polisi mjini Arusha,”anasema mwanasiasa mmoja ambaye ameona sehemu ya utetezi wa Lema akirejea taarifa ya Polisi inayoashiria kuwa waandamanaji walikaribia kabisa eneo la Polisi.

Anaongeza mwanasiasa huyo: “Taarifa ya Jeshi la Polisi (aliyonukuu Pinda bungeni) haisemi ukweli wa jinsi matukio yalivyokuwa Arusha. Kwa ushahidi wa picha za video uliopo marehemu mmoja aliuawa eneo la Mianzini ambalo liko zaidi ya kilometa tatu kutoka Kituo cha Polisi cha Arusha.

“ Aidha, marehemu wa pili alipigwa risasi katika eneo la Kaloleni ambalo nalo liko zaidi ya kilometa moja kutoka kituo hicho. Ushahidi wa video unaungwa mkono na ushahidi wa watu walioshuhudia mauaji hayo wenyewe”.

Kwa mujibu wa vyanzo kasha vya habari Lema atakosoa pia utaratibu wa jinsi Meya wa Arusha alivyopatikana, utaratibu ambao kwa mujibu wa Waziri Mkuu Pinda ni halali.

Anasema Lema katika utetezi wake kuhusu utaratibu huo:  “ Chini ya kanuni ya 8(3) ya Kanuni za Halmashauri, akidi katika mkutano wa kawaida wa mwaka na mkutano wa kwanza wa Halmashauri itakuwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri.

“ Kwa kusoma kanuni ya 8(3) pamoja na kanuni ya 9, ni wazi kwamba Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri wanatakiwa kuchaguliwa na mkutano wa kwanza wa Halmashauri.

“ Ili kukidhi matakwa ya kanuni hizi, mkutano wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Arusha ulipaswa kuwa si chini ya wajumbe 21 ambao ni theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri hiyo. Kwa maana hiyo, mkutano wa tarehe 18 Desemba haukuwa mkutano halali na viongozi wa Halmashauri
waliochaguliwa na mkutano huo hawawezi kuwa halali”.

Kipengele kingine cha utetezi wa Lema kinahusu kauli ifuatayo ya Waziri Mkuu aliposema; “Mheshimiwa Spika, yaani hata kwa hesabu tu za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza hakuna namna ambavyo kwa hali ilivyokuwa kwamba mna CHADEMA wajumbe 14, mna CCM 16,  utashindaje?”

Anajibu kauli hiyo Lema akisema: “Hapa Waziri Mkuu alitaka kuaminisha Bunge kwamba hata kama wajumbe wa CHADEMA wangehudhuria kwenye mkutano huo
bado wasingeshinda kwa sababu wajumbe wa CCM walikuwa wengi zaidi ya wajumbe wa CHADEMA”.

Anaendelea: “Lakini kwenye hotuba hiyo hiyo Waziri Mkuu alitoa kauli kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri hiyo ya Arusha: ‘ wakaingia awamu ya pili ya kumtafuta Naibu Meya, wakapiga kura, mjumbe wa kutoka TLP akashinda, CCM alishindwa hakupata kura
hata moja, CHADEMA hawakupata kura hata moja’.

“Kama iliwezekana kwa mgombea wa TLP ambaye yuko peke yake katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kupata kura za wajumbe wote wa CCM na kumshinda mgombea wa CCM
ambaye – kwa kauli ya Waziri Mkuu – hakupata kura hata moja, je, ingeshindikanaje kwa mgombea wa CHADEMA yenye wajumbe 14 kushinda?

“Swali hili ni muhimu hasa kwa vile chini ya kanuni ya 9(1) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Arusha inasema kwamba kura ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu wake itakuwa ni ya siri! Na kama inavyofahamika, katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Hai, ni mgombea wa CHADEMA ndiye aliyeshinda pamoja na kwamba CCM ina wajumbe wengi zaidi katika Halmashauri hiyo.”

Baadhi ya wabunge wa CCM waliozungumza na Raia Mwema mjini Dodoma, wamesema hakukuwa na sababu kwa Spika kumlazimisha Lema kuwasilisha ushahidi na badala yake angetumia busara zaidi kuimaliza hoja hiyo bila kuathiri pande zote.

“Spika ameteleza ama anakusudia kumdhalilisha Waziri Mkuu kwani hakuwa na haja ya kumlazimisha Lema awasilishe ushahidi maana hakuwa amesema Waziri Mkuu ni muongo bali aliomba mwongozo. Sasa ndiyo maana tena amebadili na kumtaka awasilishe ushahidi kwa maandishi,” anasema Mbunge mmoja wa CCM, ambaye ameomba asitajwe.

Picha na habari kwa hisani ya Gazeti la Raiamwema