TAARIFA ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba, idadi kubwa ya abiria wanahisiwa kupoteza maisha baada ya Meli ya LCT Spice Islanders kuzama katika Bahari ya Hindi, Pwani ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ikielekea Pemba.
Akizungumzia ajali hiyo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi amesema tukio hilo limetokea saa 8:30 za usiku ambapo meli hiyo ilikuwa imebeba abiria takribani 610 na mizigo anuai.
Haji Ussi amesema meli hiyo iliondoka katika Bandari ya Malindi Unguja ikiwa katika hali ya uzima, lakini katikati ya safari ikapata hitilafu na kusababisha kubiruka na hatimaye kuzama kabisa.
Hadi sasa haijaweza kufahamika idadi kamili ya watu waliofariki,lakini vyombo vya uokozi vimefika katika eneo la tukio kutoa msaada.
Naibu Waziri Issa amesema Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usafiri vya binafsi boti ziendazo kasi zimekwenda eneo la tukio kutoa msaada unahitajika. Jeshi la Polisi Tanzania limetuma Helkopta yake kwenye eneo la tukio.
Awali, amesema Mamlaka zinazohusika zilipata taarifa za kuzama kwa meli hiyo baada ya Meli ya Mv Jitihada inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuripoti kuzama kwa meli ya Spice Islanders ambayo ililazimika kukatisha safari yake kuelekea Kisiwani Pemba na kwenda kwenye tukio. Serikali imesema taarifa zaidi zitakuwa zikitolewa na wananchi wameombwa kuwa watulivu.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini meli hiyo ilikuwa na abiria ni 500 pamoja na wafanyakazi 12. Vyombo vya JWTZ na KMKM cha mjini Zanzibar vipo eneo la tukio kwa msaada zaidi.
Kiongozi Msaidizi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto amesimamisha ushiriki wa kampeni Igunga na sasa anaelekea Zanzibar kuungana na wananchi katika majonzi hayo.