Mazishi ya aliyekuwa Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL Marehemu Amanda Luhanga Njavike( 36) yamefanyika katika Kijiji cha Mlangali, Ludewa Mkoani Njombe.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiongozwa na Viongozi wa dini Dhehebu la Anglicana, yalifanyika majira ya sa 7 mchana siku ya Jumatatu tarehe 29 Februari, 2016 mara baada ya Ibada ya Misa ya kumuombea Marehemu.
Pamoja na idadi kubwa ya Wakazi wa Mlangali, mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Wafanyakazi wenzake wa Kampuni ya TTCL Makao Makuu na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Waombolezaji kutoka Mkoa wa Mbeya waliowasindikiza wazazi wa Marehemu, Wawakilishi wa Kampuni zinazofanya kazi na Mume wa Marehemu, Wawakilishi wa Vikundi mbali mbali ambavyo Amanda alikuwa mwanachama,Ndugu, Jamaa, na Marafiki kutoka maeneo mbali mbali ya nchi.
Katika mahubiri, Baba Askofu wa Kanisa la Anglikana alisema, Kanisa limepokea kwa huzuni taarifa za kifo cha Bi Amanda Luhanga ambaye alikuwa muumini mwaminifu wa kanisa hilo na aliyekuwa mstari wa mbele katika ibada na shughuli za Kanisa kila alipokwenda.
Kwa Upande wake Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Kampuni ya TTCL Bw Juvenali Utafu amesema, Miaka 9 ya Utumishi wa Marehemu Amanda katika Kampuni hiyo ni umeandika historia itakayodumu siku zote kutokana na nidhamu, bidii ya kazi na mchango mkubwa wa kuitangaza Kampuni hiyo kupitia taaluma yake katika fani ya Habari na Mahusiano kwa Umma.
Marehemu Amanda Luhanga Njavike alifariki dunia akiwa likizoni Mkoani Mbeya alikokwenda kuwasalimu wazazi na ndugu zake. Aliugua ghafla siku ya Alhamisi Februari 25, 2016 na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya hadi usiku wa kuamkia Jumamosi Februari 27, 2016 ambapo Mungu alimchukua.