Wataalamu TPRI Wapelekwa Kilombero Kufanya Uchunguzi

mpunga
Na Jacquiline Mrisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro imewapeleka wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viuwatilifu ya Kitropiki (TPRI) wilayani Kilombero kufanya uchunguzi wa zao la mpunga linalosadikiwa kuharibiwa na dawa zilizomwagwa na Kampuni ya Kilombero Plantation (KPL) inayomiliki mashamba yanayopakana na mashamba ya wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro Bw. Ernest Mkongo kuhusu uchunguzi unaoendelea kufanyika katika mashamba ya wananchi ili kutathmini athari zinazotokana na dawa hizo.

“Wataalamu kutoka TPRI wameshafanya uchunguzi wa awali na mpunga huo umeonekana kuwa na rangi ya njano isivyo kawaida, hivyo wamechukua sampuli za mpunga huo na kuzipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kujua kama umeharibiwa na dawa za kuondoa magugu zilizomwagwa na Kampuni ya KPL” alisema Mkongo

Aidha, Bw. Mkongo ameongeza kuwa, Taasisi ya TPRI ina wataalamu wa uhakika kwa hiyo anaamini watatoa majibu ya ukweli juu ya tatizo hilo.

TPRI ilianzishwa miaka ya 1940 ambapo kwa Tanzania ilirasimishwa rasmi katika Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Sheria Na. 18 ya mwaka 1979 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa zinazoathiri afya ya binadamu, wanyama na mazao.