Rais wa zamani wa Bayern Munich Uli Hoeness hatimaye yuko huru. Ameachiliwa huru kutoka gerezani baada ya kutumikia kifungo cha miezi 21 kwa makosa ya kukwepa kulipa kodi.
Hoeness mwenye umri wa miaka 64 alitumikia nusu ya kifungo chake cha miaka mitatu na nusu baada ya kuhukukiwa Machi 2014 kwa kukwepa kulipa kodi ya kiasi cha euro milioni 28.5. Wizara ya sheria ya jimbo la Bavaria imethibitisha kuachiliwa huru kwake bila kutoa maelezo zaidi.
Hoeness alisema atatangaza mipango yake ya baadaye mnamo Julai mosi. Tarehe ambayo Carlo Ancelotti ataanza majukumu yake kama kocha wa Bayern Munich na kumrithi Pep Guardiola. Hoeness anatarajiwa kupewa jukumu la kutekeleza katika klabu hiyo kubwa ya Ujerumani.