Waziri Mkuu Majaliwa Apokea Misaada wa Zahanati, Kompyuta

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepokea msaada wa kujenga zahanati na nyumba ya mganga kwenye kijiji cha Nandagala, wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Msaada huo wenye thamani ya dola za Marekani 55,000 (sawa na sh. Milioni 119.35) umetolewa na kampuni ya Huawei Technologies yenye makao yake jijini Dar es Salaam. Pia wametoa kompyuta za mezani (desktop) 25 pamoja na UPS 25 kwa ajili ya shule tano za sekondari wilayani humo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, Februari 28, 2016 Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei, Bw. Bruce Zhang alisema kampuni yake imetoa msaada huo ikiwa ni mwitikio wa sera ya Wizara ya Afya inayotaka kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya.

Wakati huohuo, kampuni ya mtandao wa simu ya Halotel ilimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. Milioni 9/- ambazo ni mchango wao wa kumsaidia Waziri Mkuu ambaye pia ni mbungewa jimbo la Ruangwa ili zisaidie kulipia familia zisizo na uwezo kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Akizungumza na wanakijiji hao kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Meneja Mkuu Msaidizi wa Biashara wa Mkoa wa Lindi, Bw. Sebastian Innocent alisema: “Mchango huu utazihusu kaya 900 ambazo zinalipiwa sh. 10,000 kila moja. Kila kaya inatakiwa kulipia watu sita, hivyo tutaweza kuwafikia watu 5,400 kupitia mchango huu. Alisema kampuni yao imejenga minara 50 katika mkoa wa Lindi ambapo 40 inafanya kazi na minara 22 kati ya 40 imeunganishwa na inatoa huduma ya 3G.

Akitoa shukrani kwa misaada yote, Waziri Mkuu alisema anaishukuru kampuni ya Halotel kwa kumsaidia kulipia sh. Milioni 9/- kwa ajili ya CHF ambazo alisema zimegawanywa katika vijiji 90 vya wilaya nzima ya Ruangwa na kwa kaya 10 za watu sita sita.

Aliwashukuru kwa kuweka minara katika wilaya hiyo jambo ambalo alisema litasaidia wananchi kupata mawasiliano ya simu kwa urahisi zaidi. Kuhusu zahanati, Waziri Mkuu Majaliwa aliishukuru kampuni ya Huawei Technologies kwa msaada huo ambao alisema utakapokamilika, utawapunguzia wananchi adha ya kwenda kijiji cha jirani kupata huduma ya matibabu.

Alisema ana mpango wa kuweka nguvu ya umeme jua (solar power systems) kwenye shule zote za msingi, shule zote za sekondari na zahanati zote kwenye wilaya ya Ruangwa ambayo ndiyo jimbo lake ili asiwepo mtoto wa kushindwa kusoma au mtu kupata matibabu kwa sababu ya kukosa umeme. Wilaya ya Ruangwa ina shule za msingi 82, shule za sekondari 15, vituo vya afya vitatu na zahanati 28. Waziri Mkuu alirejea Mtwara jana hiyo hiyo na leo hii amerejea Jijini Dar es Salaam.