Chuo Kikuu South Carolina Marekani kushirikiana na Chuo cha Taifa Zanzibar

Baadhi ya majengo ya Chuo Kikuu cha South Carolina cha Marekani

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

CHUO Kikuu cha Taifa cha South Carolina kiliopo Marekani, kimesema kitaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuendeleza uhusiano uliopo kati yake na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Hayo yalielezwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha South Carolina cha Marekani ukiongozwa na Rais wake Dk. George Copper wakati ulipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu Mjini Zanzibar.

Uongozi huo ulimueleza Rais Dk. Shein kuwa kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo umeamua kuendeleza uhusiano huo na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), kwa ajili ya kuandaa kozi ya Shahada ya Pili ya Uongozi wa Elimu.

Pia, uongozi huo ulieleza azma yake ya kukuza ushirikiano na SUZA ikiwa ni pamoja na kubadilishana wataalamu wakiwemo wakufunzi na wanafunzi wa vyuo vikuu hivyo kwa awamu pamoja na kusaidia vitabu kwa ajili ya maktaba ya Chuo Kikuu cha SUZA.

Katika maelezo yao viongozi hao wa Chuo Kikuu hicho walieleza kuwa wataendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu hatua ambayo itaendeleza na kukuza uhusiano uliopo kati ya Chuo hicho na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Rais wa Chuo Kikuu cha South Carolina Dr. George Copper alimueleza Dk. Shein kuwa katika Mradi wa ‘Text Book and Learning Material Program’ (TLMP) ambao hivi sasa wanashughulikia mradi kama huo huko Tanzania Bara.

Zanzibar tayari imeshafaidika na mradi huo ambao jumla ya vitabu milioni 1.2 vya masomo ya Sayansi yakiwemo Baiologia, Fizikia, Kemia na Hisabati vilichapishwa. Vitabu hivyo viliweza kuwasadia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa Sekondari kwani kila mwanafunzi alipatiwa vitabu hivyo.

Dk. Copper alimueleza Dk. Shein kuwa tayari wameshakabidhi vitabu kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi Tanzania Bara sherehe zilizofanyika hapo jana, ambapo kutokana na mashirikiano mazuri yaliopo kati yao na Zanzibar wameona haja ya kuja kuonana na Rais na kumuelezea azma yao ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu.

Aidha, ujio wao huo una lengo la kuzungumza na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika kuangalia uwezekano wa kusaidia utaalamu juu ya kuandaa miongozo ya kufundishia Elimu ya Mandaalizi.

Sambamba na hayo, uongozi huo ulieleza azma ya ujio wao ni pamoja na kuangalia matumizi ya vitabu vya Sayansi na Hisabati vya Sekondari na kupata maoni ya walimu na wanafunzi katika Skuli ya Mpapa.

Uongozi huo pia, ulimueleza Rais Dk. Shein kuwa kupitia Mradi wa TLMP wanafunzi wawili kutoka Zanzibar mmoja wa kike na mmoja wa kiume walipatiwa ufadhili wa masomo katika Chuo Kikuu hicho ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao na wanatarajiwa kurudi hivi karibuni baada ya kumaliza masomo yao.

Nae Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Chuo Kikuu chaTaifa cha South Carolina kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na misaada yake mbali mbali inayotoa kwa Zanzibar.

Dk. Shein alieleza kuwa misaada ya vitabu iliyotolewa na Chuo Kikuu hicho pamoja na inayokusudia kutolewa ni chachu ya maendeleo katika sekta ya elimu hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa elimu ni jambo muhimu na katika vipaumbele vilivyowekwa na serikali ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu hivyo hatua ya kusaidia vitabu pamoja na vifaa itaimarisha sekta hiyo.

Dk. Shein alieleza kuwa hatua ya kusaidia utaalamu juu ya kuandaa miongozo ya kufundisha Elimu ya Maandalizi itasaidia katika kutimiza lengo la serikali la elimu ya msingi ianzie maandalizi kwani walimu wake watapata elimu bora ya kufundishia.

Aidha, Dk. Shein aliupongeza uongoziwa chuo hicho kwa juhudi kubwa unazozichukua katika kuunga mkono sekta ya elimu Zanzibar na kueleza kufarajika kwake na hatua hiyo kwa Zanzibar na Tanzania Bara kwa jumla.

Alieleza kuwa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania vitabu na vifaa vya masomo katika skuli na vyuo ni vitu muhimu sana katika kuendeleza elimu hatua ambayo imeweza kuwasaidia wananfunzi wengi wa sskuli za Sekondari Zanzibar kufanya vizuri katika masomo yao ya sayansi, hiyo ni kutokana na msaada wa vitabu kutoka chuo hicho.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina mikakati kabambe ya kukiimarisha Chuo Kikuu cha SUZA, hivyo mashirikiano yake na Chuo Kikuu cha Taifa cha South Carolina kutakuwa chachu ya mikakati hiyo.

Katika Ujumbe huo wa viongozi kutoka Chuo Kikuu cha South Carolina mbali ya Rais wa Chuo hicho alikuwemo Dk. Leonard McIntyre Mkurugenzi wa Mradi wa Uandishi wa vitabu vya Sayansi na Hisabati (TLMP), Bwana Lamin Drammeh Maneja wa Mradi wa uandishi wa vitabu vya Sayansi na Hisabati na mke wa Rais Bibi Diane Copper.