Samatta Atupia Bao lake la Kwanza Akitokea Benchi

Samatta-Genk

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefunga bao lake la kwanza katika klabu yake mpya, KRC Genk katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji wakishinda 3-2 dhidi ya Club Bruge Uwanja wa Cristal Arena, Genk.

Samatta aliyejiunga na Genk Januari akitokea TP Mazembe ya DRC, alifunga bao hilo dakika ya 81 akimalizia pasi ya kiungo Ruslan Malinovskiy, baada ya kuingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Nikolaos Karelis dakika ya 79.

Na Samatta aliyekuwa akicheza mechi yake ya tatu leo tangu ajiunge na Genk, angeweza kufunga tena kama kama si shuti lake kupanguliwa na kipa wa Bruge mwishoni kabisa mwa mchezo.

Mabao mengine ya Genk yamefungwa na Karelis kwa penalti dakika ya 36 na Thomas Buffel dakika ya 50, wakati ya Bruge yamefungwa na Thomas Meunier dakika ya 15 na Hans Vanaken dakika ya 83.

Na ushindi huo, unaifanya Genk ifikishe pointi 45 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kukamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Na binzubeiry.com