Tanzania kuiuzia Kenya tani 10,000 za mahindi

Na Mwandishi Maalumu

TANZANIA na Kenya zimekubaliana kukomesha biashara ya miaka mingi ya magendo ya chakula kwenye mpaka wa nchi hiyo kwa kuamua kuuziana chakula rasmi kwa njia halali kuanzia sasa. Kwa kuanzia, Tanzania imekubali kuiuzia Kenya tani 10,000 za mahindi ili kuiwezesha nchi hiyo kukabiliana na baa la njaa linalowakabili mamilioni ya wananchi wa Kenya hasa katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.

Makubaliano hayo ya aina yake baina ya nchi za Afrika yamefikiwa leo, Ijumaa, Septemba 9, 2011, mjini Nairobi, Kenya wakati wa mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Mwai Kibaki wa Kenya.

Mkutano kati ya Rais Kikwete na Rais Kibaki umefanyika pembeni mwa mkutano wa siku mbili wa kimataifa wa kujadili zahama ya ukame na baa la njaa katika nchi za Pembe ya Afrika uliomalizika leo mjini Nairobi.

Rais Kikwete aliwasili Nairobi jioni ya jana, Alhamisi, Septemba 8, 2011, kuhudhuria mkutano huo ambao kwa leo umewakutanisha wakuu wa nchi za eneo hilo kwenye eneo la Umoja wa Mataifa, Gigiri, nje kidogo ya Nairobi.

Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete na Rais Kibaki, wametafakari faida za kuanzisha biashara rasmi ya kuuziana chakula baina ya nchi hizo mbili na umuhimu wa kukomesha magendo ya chakula ambayo imekuwa inafanyika kwa miaka mingi katika mpaka wa nchi hizo.

Katika miezi ya karibuni imekuwapo magendo makubwa ya chakula, na hasa mahindi, kutoka Tanzania ambako makumi kwa makumi ya malori ya chakula cha magendo yamekuwa yakivushwa mpaka kuingia Kenya ambayo baadhi ya sehemu zake zinakabiliwa na baa la njaa.

Kiasi cha wananchi milioni 3.7 wa Kenya, wakiwamo wakimbizi 477,000 kutoka Somalia wanakadiriwa kukumbwa na ukame na hivyo kuhitaji msaada wa chakula na misaada mingine ya kibinadamu kaskazini mwa nchi hiyo.

Chini ya makubaliano kati ya Rais Kikwete na Rais Kibaki, nchi ya Kenya itatakiwa kutathmini mara moja mahitaji yake ya chakula na kuiarifu Tanzania ambayo kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na hasa kupitia taasisi ya chakula cha akiba ya SGR itafanya maandalizi ya kuuza chakula hicho kwa Kenya.

Ujumbe wa Kenya unatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo ukiwa na takwimu za mahitaji yake tayari kwa mazungumzo na maofisa wa Tanzania wanaoshughulika na masuala ya chakula na biashara.

Katika mazungumzo hayo, maofisa hao pia watakubaliana utaratibu wa kukisafirisha chakula hicho, wasafirishaji wenyewe wa chakula na njia zitakazotumika katika kukisafirisha kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kukipeleka Kenya.

Miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) Tanzania ni nchi pekee yenye akiba ya chakula, na hasa mahindi, wakati nchi nyingine zilizobakia za jumuia hiyo zinakabiliwa na njaa na ukosefu wa chakula kwa viwango vinavyotofautiana.

Tanzania imekuwa inajitosheleza kwa chakula kwa miaka mitatu iliyopita bila kulazimika kuagiza chakula kutoka nje na kimsingi hayo ni matokeo ya sera ya sasa ya Serikali ya kutoa ruzuku ya mbegu, mbolea, dawa za kuulia wadudu na mahitaji mengine ya kilimo kwa wakulima.

Ruzuku hiyo, kimsingi imekuwa inatolewa kwa wakulima kwa mikoa inayozalisha chakula, na hasa mahindi, kwa wingi. Ruzuku hiyo ilianza kutolewa kwa mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma na Rukwa hata kama mikoa sita inayozalisha chakula kwa wingi inashirikisha pia mikoa ya Morogoro na Kigoma.