Mafunzo Fc Mguu Pande Kuikabili AS Vita Ligi ya Mabingwa Afrika

MAFUNZO-FC

Timu ya soka ya Mafunzo, kimeondoka Zanzibar jana kwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tayari kwa pambano la marudiano dhidi ya AS Vita ya huko mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Walinzi hao wa wafungwa wameondoka kwa ndege ya Shirika la Ethiopian Airline saa nane mchana jana baada ya awali kuagwa na Mwinyi Jamal Ramadhan kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Kanali Mstaafu Abdi Mahmoud Mzee katika ukumbi wa makao makuu ya Vyuo vya Mafunzo, Kilimani mjini hapa.

Timu hiyo imeondoka ikiwa na deni la mabao 3-0, ikihitaji ushindi wa kuanzia 4-0 ili iweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Februari 13, 2016 uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, wajelajela hao walilala kwa mabao 3-0.

Mapema, akiwaaga wanandinga hao, katika hafla iliyofanyika jana asubuhi, Jamal aliwataka kuzingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja pamoja na kujituma kikamilifu ili waweze kubadilsa matokeo kwa manufaa yao na wapenda soka wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

“Katika jambo lolote ikiwemo michezo, nidhamu ndio kitu cha msingi kama mtu anataka kupata mafanikio. Nendeni mkapambane lakini hakikisheni pambao lenu haliwatoi katika uanamichezo na kusahau kutunza nidhamu,” alisisitiza Jamal.

Aidha, alisema licha ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani, bado timu hiyo ina nafasi ya kushinda kwa idadi nzuri ya mabao na kusonga mbele kwenye mashindano hayo.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya soka Zanzibar msimu wa 2015/2016 wanaonolewa na Hemed Suleiman ‘Moroko’, wanatarajiwa kushika uwnajani mjini Kinshasa Jumapili ijayo kumenyana na wenyeji wao, AS Vita. Habari na Binzubeiry.com