TUME ya Uchaguzi nchini Uganda imemtangaza Rais Yoweri Museveni kuwa ni mshindi wa Uchaguzi wa Urais uliofanyika Alhamisi iliyopita. Kwa mujibu wa tume hiyo Rais Museveni alipata kura 5,617,503 sawa na asilimia 60.75 ya kura zilizohesabiwa kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo Dk. Badru Kiggundu.
Mpinzani wake mkuu Dk. Kizza Besigye alipata kura 3,270,290 ambazo ni sawa na asilimia 35.37. Museveni ametangazwa mshindi licha ya kwamba kuna vituo ambavyo bado matokeo hayajatangazwa. Dk. Kiggundu amesema matokeo ya vituo hivyo hayawezi kubadilisha mambo.
Hata hivyo wapinzani wake Dk. Besigye na Muntu wameachiliwa huru tayari baada ya kuwa wakishikiliwa nchini Uganda. Awali, waangilizi kutoka Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Madola walikuwa wamekosoa uchaguzi huo wakisema kulikuwa na kasoro nyingi. Aidha walishutumu kukamatwa kwa mgombea wa upinzani Dkt Besigye na kuzimwa kwa mitandao ya kijamii.