Prof. Tibaijuka acharuka, afuta viwanja 87 vilivyovamiwa

Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeanza kufanya oparesheni maalumu kuhakikisha inayarejesha maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa kinyemela maeneo ya Jiji, Miji na katika manispaa.

Zoezi hilo linafanywa kwa kusimamiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazia, Prof. Anna Tibaijuka, ameanza katika majiji, miji na Manispaa, na tayari Wizara imefuta hati za viwanja 82 zilizotolewa kinyemela.
Akizungumza na vyombo vya habari jana Dar es Salaam, Prof. Tibaijuka amesema wizara yake itahakikisha mabadiliko yoyote ya ardhi yaliofanywa bila utaratibu unaofaa yanabatilishwa ili kurejesha hadhi ya miji.

Alisema kufuatia zoezi hili maeneo muhimu ya wazi ambayo yamefutiwa hati jijini Dar es Salaam ni Mikocheni vilipokuwa vimepimwa viwanja 12 eneo ambalo lilikuwa chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).

“Eneo la mabwawa ya maji taka Mikocheni lilikuwa limevamiwa na kupimwa viwanja 12.., maeneo mengine ambayo nimefuta hati ni Mbezi hati 30, na Moshi eneo la Sekondari la Weruweru 40,” alisema Waziri Tibaijuka.

Hata hivyo amesema licha ya wizara kufuta hati hizo lipo suala la kibinadamu hivyo inahakikisha wananchi wanapewa taarifa kwani wapo ambao walitapeliwa na huenda wakafanikiwa kupewa viwanja vingine na Serikali.

“Mtu yeyote anayefikiria kuishi kwa ujanja akiamini atapata hati kinyume na utaratibu kwa sasa, itakuwa ngumu kama ilivyotokea katika eneo la Masaki maana hati zote feki zinaishia katika dawati langu nazifuta,” alisema Waziri huyo.

Aidha aliongeza kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi baadhi ya halmashauri, wizara ipo mbioni kuzipokonya madaraka halmashauri zilizokithiri kwa migogoro hiyo-hali ambayo itaifanya manispaa husika kufanya kazi kwa ushirikiano na wizara. “…mfano Jiji la Dar es Salaam lina ‘master plan’ ambayo inakwenda na sheria, halmashauri inakasimiwa madaraka na Wizara, hivyo zisipofuata utaratibu inanyang’anywa na hata suala la kulinda maeneo ya wazi ni la utawala bora,” alisema Tibaijuka.