Na Bashir Nkoromo, Igunga
MWENYEKITI mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amewasili Igunga jana jioni kwa ajili ya kufungua kampeni za CCM za ubunge katika Jimbo la Igunga, zinazotarajiwa kufanyika Jumamosi hii.
“Nimewasili Igunga, wana-Igunga kazi ni moja, ni ushindi tu, alisema Mkapa akisalimia wananchi baada ya kupokewa katika kijiji cha Makomero kilometa nane kutoka mjini Igunga mkoani Tabora.
“Nashukuru sana kuona kwamba mara hii nimefika hapa Igunga kwa kupita barabara ya lami, mara ya mwisho nilipita kukiwa vumbi tu, jamani haya si maendeleo? alisema Mkapa huku akishangiliwa na wananchi.
Mkapa aliwataka wananchi wa Igunga kujitokeza kwa wingi Oktoba 2, mwaka huu kupiga kura na kuhakikisha wanampigia mgombea wa CCM Dk. Dalaly Peter Kafumu, akisema kufanya hivyo watakuwa wamechagua maendeleo.
“Lamsingi ni hilo mengine nitawaambia tutakapokutana katika mikutano ya kampeni, yapo mengi sana,” alisema Mkapa.
Katika mapokezi hayo, Mkapa alipokelewa na viongozi mbalimbali wa CCM, waliongozwa na Mratibu wa Kampeni za CCM jimboni humo, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba, Katibu wa NEC, Oganaizesheni Asha Abdallah Juma na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Hassani Wakasuvi.
Baada ya kusalimia mwananchi msafara wa Mkapa ulikwenda mjini ukiwa na magari kadhaa, yaliyozungumwa na vijana waendesha pikipiki na baiskeli.
Kabla ya kuzindua kampeni za CCM, katika viwanja vya Kumbukumbu ya Samora mjini Igunga,leo Mkapa atakuwa na shughuli mbalimbali za kampeni na baada ya uzinduzi wa kampeni hizo ataendeleo na mikutano kesho yake.