Dk. Kigwangalla Kuyasaka ‘Majipu’ Hospitalini, Zahati na Vituo vya Afya

Dk. Hamis Kigwangalla

Dk. Hamis Kigwangalla

Magreth Kinabo, Maelezo

SERIKALI imesema itaangalia upya mikataba iliyopo ya vifaa vya maabara vilivyoko katika hospitali, zahati na vituo vya afya nchini ambavyo havifanyi kazi ili kama ni jipu litumbuliwe na wahusika wachukuliwa hatua.

Kauli hiyo ilitolewa Februari 16, 2016 na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla mara baada ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro na kuhitimisha yaliyojili katika ziara yake ya kikazi kwenye mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa, ambapo alitembelea baadhi ya hospitali na vituo vya afya.

Dk. Kigwangalla alizitaja baadhi ya mashine zilizokutwa hazifanyikazi katika maabara ni MRHL-014 (CL- CHEMISRTY SECTION), BIOCHEMISTRY, FULLBLOOD PICTURE, kwa sababu ya kutofanya kazi au kukosa vitenganishi (reagents).

“Nimetembelea mikoa mitano nimebaini kuwa hospitalini kote nilikozunguka mashine hazifanyikazi, na nimegundua kwamba msambazaji wa mashine hizo ni mmoja na ndiye anayehusika na vitenganishi. Msambazaji huyo ni Bohari Kuu ya Dawa (MDS). Hospitali zote zina akaunti MSD na Hawawezi kupewa fedha wakanunua vitenganishi bali wanavipata MSD.

“Nitafanya uchunguzi kwa kusoma mkataba kwa kina baina ya MSD na kampuni ya Biocare ambayo inahusika na vifaa hivi, kwanini vitenganishi vitolewe na MSD na vifaa viwe ni vyake pia tutaenda kuchunguza kati MSD na Kampuni ya Biocare kuna nini ili kama ni jipu litumbuliwe,” alisema Dk. Kigwangalla.

Hata hivyo naibu Waziri huyo ameisifia maabara ya hospitali hiyo, na kusema ni nzuri, ila tatizo mashine zake hazifanyikazi na mazingira ya hospitali hiyo sio mazuri, baadhi ya maeneo kuna bubui, vyoo ni vichafu, taa zilizoko katika vyumba vya upasuaji hazifanyi kazi na zinazotumika sio zinazotakiwa, mfumo wa mtandao uko katika eneo la utumishi wa usajili, na jengo la kulipia haliko katika ubora unaotakiwa.

Aidha Dk. Kigwangalla alimwagiza, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Rita Lyiyamuya kuhakikisha mapungufu yanafanyiwa marekebisho hayo, ambapo alitoa muda wa siku 60 wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Morogoro. Pia alitoa muda wa miezi sita wa kufanya marekebisho ya baadhi ya majengo likiwemo la wodi za kulipia ili yawe katika ubora unaotakiwa.

Aliutaka pia uongozo wa hospitali hiyo kufunga mtandao wa ukusanyaji mapato katika sehemu zote ili kuepusha upoteaji wa mapato ambayo yanaweza kusaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya katika hospitali hiyo.

Alisema pia Serikali itaanzisha utaratibu wa kuhakikisha kila mtu anapata huduma za matibabu ya afya kwa kutumia mifuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)na mfumo wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) kama ilivyo kwa leseni au utoaji wa vibali mbalimbali.