JK apokea hati za mabalozi

Jengo la Ikulu ya Tanzania.

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete leo asubuhi amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi wa Australia, Finland, Mexico na Misri. Mabalozi Geoffrey Peter Tooth wa Australia na Balozi Luis Javier Campuzano wa Mexico watakuwa na makazi yao jijini Nairobi wakati Balozi Sinikka Antila wa Finland na Hossam Eldin Moharam wa Misri watakuwa na makazi yao hapa jijini Dar es Salaam.

Mapema kabla ya kupokea Hati za Utambulisho za mabalozi hao Rais Kikwete amekwenda kenye makazi ya balozi wa Cuba hapa nchi, ambapo ametia saini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Makamu wa Rais wa Cuba, Jenerali Julio Casas Regueiro.

Wakati huo huo Rais Kikwete mchana huu anatarajiwa kuelekea Nairobi , Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku moja, kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais Mwai Kibaki wa Kenya.

Akiwa Nairobi, Rais Kikwete anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Kimataifa kuhusu Ukame Ulioathiri Nchi za Pembe ya Afrika.
Mkutano huo utakaoongozwa na Rais Kibaki, unatarajiwa pia kuhudhuriwa na viongozi kutoka Djibouti, Ethiopia, Somalia, Uganda, Sudan na Sudan Kusini.

Mkutano pia utahudhuriwa na viongozi wa Taasisi za Kimataifa ambazo ni Umoja wa Afrika (AU) Umoja wa Mataifa (UN), Mwenyekiti wa Benki ya Dunia na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Umoja wa Mataifa.
Rais Kikwete anatarajiwa kurejea kesho mara baada ya kikao hicho kumalizika.

Imetolewa na Premi Kibanga, Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Ikulu.