CAG kukagua vocha za kilimo nchi nzima

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Ludovick Utouh

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Serikali nchini (CAG) ameagizwa kufuatilia usambazaji wa vocha za pembejeo nchi nzima ili kubaini kama zinawanufaisha wakulima au la.

Agizo hilo limetolewa jana Septemba 7, 2011 na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akizungumza na viongozi wa mkoa wa Rukwa na wa wilaya ya Mpanda mara baada ya kuwasili katika kiwanja kidogo cha ndege cha Sitalike wilayani Mpanda.

Akipokea taarifa za Mkoa na Wilaya eneo hilo, Waziri Mkuu alisema suala la vocha limegubikwa na wizi mkubwa unaofanywa baina ya mawakala na watendaji hivyo kutaka ukaguzi ufanywe.

“Kwenye vocha kuna wizi wa makusudi. Ukifuatilia utabaini zinaletwa vocha nyingi na zinasambazwa karibu asilimia 90 lakini je ni kweli zimekwenda kwa wakulima wa kawaida au zinatumika kusaidia mlanguzi?” alihoji.

Alisema bado kuna changamoto kubwa katika suala zima la vocha na Serikali inatafuta njia mbadala itakayosaidia kuhakikisha kwamba vocha hizo zinawasaidia wakulima wadogo kuboresha mfumo wao wa kilimo.

Alisema kuna baadhi ya maeneo watu wamekamatwa na kuchukuliwa hatua lakini bado kuna ‘kamchezo’ kanaendelea baina ya watendaji wasio waaminifu na mawakala na ndiyo maana Serikali imemwagiza CAG afanye ukaguzi katika eneo hilo.

“Viongozi wa mkoa na wilaya bado mna changamoto ya kuwabana mawakala … simamieni zoezi hili vizuri ili kuhakikisha tunawafikia walengwa,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu mahitaji ya mbolea, Waziri Mkuu alisema hali si mbaya kwa sababu Serikali imekwishaagiza mbolea ya kutosha bali aliwataka viongozi hao waangalie uwezekano wa kubadili msimu wa mauzo ya mbolea ili wauze mbolea wakati mazao yananunuliwa.

“Kama mtu angetaka kununua mbolea leo hii angeweza kwa sababu angetumia fedha anayopata kwa kuuza mahindi papo hapo, lakini msimu wa ununuzi ukishapita, si rahisi watu kuwa na fedha za kununulia mbolea,” alisema.